Sep 11, 2023 14:01 UTC
  • Msikiti wa al-Aqswa ni mstari mwekundu wa taifa la Palestina

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS huko Quds iinayokaliwa kwa mabavu ameashiria vitendo vya Wazayuni vya kulivunjia heshima eneo hilo takatifu na kusisitiza kwamba, msikiti wa al-Aqswa utaendelea kuwa mstari mwekundu wa taifa la Palestina.

Muhammad Hamada amesisitiza kwamba, jinai mtawalia za wavamizi na walowezi wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqswa zinazidi kuimarisha moyo wa muqawama na mapambano dhidi ya maghasibu. 

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa, msikiti wa al-Aqswa utaendelea kubakia kuwa mstari mwekundu wa Waislamu na kwamba, kila mkono wenye lengo la kuuvunjia heshima msikiti huo utakatwa.

Israel inashadidisha vitendo vyake haramu na kubadili muundo wa kijiografia na kijamii wa mji wa Quds sambamba na kufuta utambulisho na utamaduni wa Kiarabu kupitia mipango yake ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na miundomsingi inayohusiana na vitongoji hivyo ikiwemo na kujenga barabara na njia ya chini kwa chini.

Hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqswa vimekithiri zaidi baada ya kuingia madarakani serikali yenye misimamo mikali ya Benjamin Netanyahu ambayo imekuwa ikionyesha chuki za wazi wazi dhidi ya Wapalestina na maeneo yao matakatifu.

Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.

Tags