Sep 18, 2023 12:19 UTC
  • Njama za Marekani za kuongeza uwepo wake wa kijeshi nchini Yemen

Tangu mazungumzo kati ya Yemen na Saudi Arabia kuhitimisha vita yalipochukua mkondo wa azma ya kweli, harakati za kijeshi za Marekani na Uingereza nazo zimeongezeka na kuimarika ili kuimarisha uwepo wao wa kijeshi katika nchi hiyo.

Licha ya kuwa Marekani ilitakiwa kukomesha uwepo wake wa kijeshi huko Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) au angalau ipunguze ili kuongeza uwepo wake wa kijeshi katika Asia ya Mashariki ili kuidhibiti China, lakini katika miezi ya hivi karibuni, Washington imefanya juhudi za kuimarisha uwepo wake wa kijeshi katika Asia ya Magharibi, ambapo sehemu kubwa ya mpango huo inahusiana na pwani ya Yemen.

Al-Azi Rajeh, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema katika mahojiano na shirika la habari la Al-Ma'louma kwamba, madhumuni ya kweli ya uwepo wa Marekani katika Taiz, Hadhramaut na baadhi ya maeneo mengine ya Yemen ni kudhibiti maeneo ya mafuta ya Yemen na kusema: Vikosi vya Marekani vinavyokuja baharini vipo katika vituo vya Marekani kwa ajili ya kushirikiana na serikali ya Abd Rabbuh Mansour Hadi, rais aliyejiuzulu wa Yemen kuimarisha wizi na uporaji wa mafuta ya Yemen.

Pamoja na hayo kuna nukta zingine kadhaa zinazoweza kuashiriwa kama msukumo wa hilo:

Nukta ya kwanza ni kwamba, kabla ya Marekani kuingia Asia Mashariki kwa ajili ya kuidhibiti China, Beijing ilishaitangulia Washington kwa kuimarisha uwepo wake katika eneo hili kabla ya Marekani kuondoka Asia Magharibi. China ilitiliana saini mikataba ya kimkakati na mataifa mengi ya eneo hili na hata Saudia ambayo wakati huo ilikuwa muitifaki muhimu wa Marekani katika eneo.

Kwa muktadha huo, inaonekana kuwa moja ya malengo ya Marekani ya kurejea katika eneo hili ni kuzuia ushawishi na uwepo wa China katika eneo hili na kukwamisha utekelezwaji wa makubaliano ya kistratijia ya China na nchi za Kiarabu za eneo hili ikiwemo Saudi Arabia. Ni kwa msingi huo ndio maana Marekani wakati wa mkutano wa hivi majuzi wa kundi la 20 nchini India, ilijaribu kupendekeza mpango wa kuanzishwa kwa daraja unganishi la reli na bahari kati ya India na Ulaya kupitia nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na pia utawala wa Kizayuni, ili kwa njia hiyo ilete mpango mbadala na ule wa China.

Sehemu ya juhudi za Marekani za kuimarisha uwepo wake wa kijeshi kwenye mwambao wa Bahari Nyekundu na kuanzisha kituo kusini mwa Yemen zinaweza kutathminiwa na kuchambuliwa katika fremu hiyo.

 

Nukta ya pili ni kuwa, katika uhusiano wa kimataifa na wa kikanda, umuhimu wa jiografia ya kisiasa na na ya kiuchumi ya Yemen umeongezeka zaidi. Yemen ina eneo la kipekee na la kuvutia sana la kijiografia, ambalo linaifanya kuwa muhimu kimkakati kwa kupitisha meli zinazotoka Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Hindi. Ukweli wa mambo ni kuwa, Yemen ni njia ya kufikia Asia na Mashariki ya Kati.

Kuna nukta 14 za kimkakati duniani, 7 kati yake ziko Mashariki ya Kati ambazo ni Malango Bahari ya Bosphorus na Dardanelles, Mfereji wa Suez, Lango Bahari la Gibraltar (Jabal Tariq), Lango Bahari la Bab al-Mandab, Tomb Kubwa na Tomb Ndogo, Lango Bahari la Hormuz na Kisiwa cha Bumusa.

Mashariki ya Kati imezungukwa na bahari tano muhimu za ulimwengu: Bahari ya Mediterania, Ghuba ya Uajemi, Bahari Nyekundu, Bahari Nyeusi na Bahari ya Caspian, wakati mataifa ya nje ya ulimwengu yanaiita Ghuba ya Uajemi kuwa ni moyo wa dunia na moyo wa nishati ya dunia.

Nukta ya tatu; tajiriba na uzoefu unanyesha kuwa Marekani daima inaitazama Asia Magharibi kupitia kioo cha maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na daima imekuwa ikitanguliza mbele zaidi maslahi ya utawala huo mbele ya maslahi yake.

Kwa mtazamo huu, kwa upande mmoja utawala huu unajaribu kuwepo katika visiwa vya kistratijia vya Yemen, kama vile Socotra, ili uweze kuongeza kipengele cha usalama wa baharini na kwa upande mwingine, kutumia maeneo haya kuhatarisha usalama wa wengine. Kwa mtazamo huo, kutumwa vikosi vya Marekani katika pwani ya Yemen na kujaribu kuanzisha kituo cha kijeshi katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo kunakwenda sambamba na sera na maslahi ya utawala wa Kizayuni.

Tags