Saudia: Suluhisho pekee la suala la Palestina ni kuundwa nchi huru ya Palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan ambaye ameelekea New York kushiriki mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema, suluhisho pekee la kadhia ya Palestina ni kuundwa nchi huru ya Palestina.
Kwa mujibu wa IRNA, Faisal bin Farhan ameeleza hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya serikali ya Saudia mjini New York na kuongeza kuwa: "Hakuna njia yoyote ya kutatua mgogoro kati ya Palestina na (utawala) wa Israel bila ya kuundwa nchi huru ya Palestina".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia ameongeza kuwa, mashauriano yanaendelea na Umoja wa Ulaya, Misri na Jordan kuhusu njia ya kulipatia ufumbuzi suala la Palestina.

Siku ya Jumapili, afisa mmoja katika ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu alisema kuwa Riyadh imeifahamisha Washington kwamba itasimamisha mazungumzo yoyote yanayohusiana na kuanzisha uhusiano na Tel Aviv au kuchukua hatua yoyote kwa ajili ya kufanikisha suala hilo.
Shirika la Redio na Televisheni la Kizayuni (Makan) pia liliripoti siku chache zilizopita likimnukuu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken kwamba ameeleza kwamba: "Wasaudi wametuambia kwa uwazi kabisa kwamba suala la Palestina ni suala muhimu na la msingi kwa ajili ya kuanzisha uhusiano na Israel; na kwa mtazamo wa Riyadh kuanzisha uhusiano inapasa kujumuishe utekelezaji wa suluhisho la serikali mbili.../