Sep 24, 2023 06:48 UTC
  • Yemen miaka 9 baada ya Septemba 21, 2014; kuanzia vitani hadi kwenye uundaji wa serikali yenye mafanikio ya Ansarullah

Miaka 9 imepita tangu Septemba 21, 2014 na kufikiwa makubaliano ya Ansarullah na serikali ya Abd Rabbu Mansour Hadi, ambapo hali ya kisiasa ya Yemen imebadilika sana.

Katika muongo mmoja uliopita,Yemen imepitia misukosuko na migogoro mingi ambapo hali ya sasa ya nchi hiyo inatofautiana sana na ya mwaka 2011. Mwaka 2011 Wananchi wa Yemen walianzisha muamko na mapambano na hatimaye wakafanikiwa kuiangusha serikali ya Ali Abdullah Saleh. Mwezi Februari 2012 walimchagua Abd Rabbu Mansour Hadi kuwa rais wa nchi hiyo katika uchaguzi wa kimaonyesho tu wa mgombea mmoja lakini baadaye Septemba mwaka 2014 wakaamua kuipindua serikali hiyo. Mwaka 2014, Wayemen walifanya maandamano katika maeneno mbalimbali ya nchi kulalamikia kushindwa siasa za serikali ya Abd Rabbu Mansour Hadi ndani na nje ya nchi na kutotumiwa vizuri utajiri na rasilimali za nchi yao. Maandamano hayo yalimalizika kwa mafanikio Septemba 21 mwaka huo huo. 

Kushadidi malalamiko dhidi ya Mansour Hadi, ambaye aliongezewa muda wa miaka miwili kinyume cha sheria, kulimpelekea kufikia makubaliano na Ansarullah ya Yemen kwa niaba ya mamilioni ya waandamanaji wa nchi hiyo. Mansour Hadi ambaye hakufurahishwa na suala la kugawana madaraka na Ansarullah, alikimbilia Saudi Arabia mwanzoni mwa mwaka 2015 na hivyo kuanda uwanda wa mashambulizi ya Saudia dhidi ya Yemen. Mansour Hadi na serikali ya Riyadh walidhani kwamba wangeweza kuwaondoa Ansarullah madarakani kwa muda mfupi na hivyo kuandaa mazingira ya Hadi kurejea tena madarakani. Ama licha ya kupita takriban miaka 9 tangu makubaliano ya Septemba 21 na miaka 8 na nusu ya vita hivyo, si tu kwamba Riyadh na Mansour Hadi hawajafikia malengo yao bali sasa Yemen inashuhudia mabadiliko makubwa. 

Magwaride ya kijeshi Yemen

Tofauti ya kwanza ni kwamba miaka 9  tokea makubaliano ya Septemba 21, Abd Rabbu Mansour Hadi hana nafasi yoyote katika muundo wa utawala wa Yemen na aliondolewa madarakani na Wasaudi wenyewe ambapo hadi sasa hajapata fursa ya kurejea kuishi Yemen.

Tofauti ya pili ni kwamba Ansarullah na waitifaki wake wameunda serikali huko Sana'a, mji mkuu wa Yemen, ambayo imejiimarisha kisiasa na kuleta mshikamano na mfungamano mkubwa nchini. Hivi sasa, Mansour Hadi na Saudi Arabia sio tu wameshindwa kuwaondoa Ansarullah madarakani, bali Ansarullah wameunda serikali na kurudisha amani na usalama nchini. Kuhusiana na suala hilo, Seyyed Abdul Malik Badr al-Din al-Houthi, kiongozi wa Ansarullah ya Yemen alisema katika kuadhimisha mwaka wa tisa wa makubaliano ya Septemba 21 kuwa kabla ya mapinduzi, nchi hiyo haikuwa na amani kabisa na Sanaa ilikuwa imebadilishwa kuwa kitovu cha  uhalifu, mauaji na milipuko. Makundi ya kitakfiri yalikuwa yamejipenyeza katika maeneo mengi ya nchi na kudhibiti kila kitu vikiwemo vyanzo muhimu vya mapatao ya taifa kama mafuta na gesi. Alisema wakati huo uchumi ulikuwa umezorota kabisa lakini leo Yemen ni huru na imeimarika kiusalama. 

 

Seyyed Abdul Malik Badr al-Din al-Houthi, Kiongozi wa Ansurallah Yemen

Tofauti ya tatu ni kwamba serikali ya Sanaa ambayo inafungamana na Ansarullah imejiimarisha na kupata nguvu kiasi kwamba Saudi Arabia imelazimika kukaa nayo kwenye meza ya mazungumzo na kujadiliana nayo suala la kusimamisha vita. Sehemu ya nguvu hiyo ilionyeshwa katika gwaride la jeshi la Yemen lililofanyika Septemba 21. Katika gwaride hilo la kijeshi, wanajeshi wa Yemen walionyesha zana zao nzito zikiwemo za kisasa kabisa na kuweka wazi kwa mara ya kwanza uwezo wao wa anga. Katika gwaride hilo na kwa mara ya kwanza, mabomu  ya baharini aina ya Saqib, Karrar, Mujahid 1, Mujahid 2 na Mujahid 3 yaliyotengenezwa nchini pia yalizinduliwa. Katika gwaride hilo la kufana la jeshi la Yemen, makombora ya kisasa ya wanamaji, kombora la Rubij na makombora ya balestiki ya Faliq na Mandab 1 yalizunduliwa na kuwekwa mbele ya watazamaji. Vilevile vikosi vya jeshi la Yemeni kwa mara ya kwanza vilionyesha kombora la masafa marefu la Sijil lenye kutumia fueli mango. Vikosi vya Yemen pia vilizindua kombora jipya la masafa marefu la Sayyad ambalo hutumia fueli mango na oevu na wala halionekani kweye rada.

Tofauti ya nne ni kwamba, kinyume na mwaka 2014, Yemen ni nchi huru inayojitegemea na haiko chini ya udhibiti wa nchi yoyote ya eneo ua nje ya eneo. Kiongozi wa Ansarullah pia amesema kuhusiana na jambo hilo kwamba  Mapinduzi ya Septemba 21 ni moja ya mafanikio makubwa ambayo Mwenyezi Mungu amewatunukia Wayemen kwa sababu yaliwatoa chini ya udhibiti wa madola mengine. Kabla ya mapinduzi hayo, Wamarekani walikuwa wanatekeleza siasa za uhasama dhidi ya Sanaa ambazo zilikuwa zinapelekea nchi hiyo kushindiwa kujisimamia katika nyanja zote. Wamarekani walikuwa wakitumia tofauti za kisiasa ili kujimarisha na kujinufaisha wao wenyewe lakini leo Yemen ni nchi huru na haiko chini ya utawala wa Marekani au nchi zingine.