Oct 01, 2023 02:38 UTC
  • Qatar yataka vituo vya nyuklia vya Israel vikaguliwe na IAEA

Qatar imetaka vituo vya nyuklia vya utawala wa Israel viwe chini usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) huku utawala huo ukiendelea kupuuza kanuni za kimataifa za nyuklia.

Ombi hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia Silaha ya Qatar, Abdulaziz Salmeen al-Jabri, katika mkutano mkuu wa mwaka wa IAEA, unaoendelea hivi sasa mjini Vienna. Shirika rasmi la Habari la Qatar (QNA) limemnukulu al-Jabri pia akitoa wito kwa utawala wa Israel ujiunge  na Mkataba wa Kuzuia Usambazaji wa Silaya za Nyuklia (NPT).
Afisa huyo wa Qatar ameeleza kwamba haya yalikuwa matakwa  halali ambayo yamesisitizwa pia na "maazimio ya kimataifa ambayo yalipitishwa nusu karne iliyopita." 
Ametaja baadhi ya maazimio hayo kuwa ni "maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa [ambayo yamepitishwa] tangu 1974, Maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa 487 ya 1981 na 687 ya 1991, maazimio mengi ya IAEA, na azimio la Mkutano wa Mapitio ya Mkataba wa Kuzuia Uenezi wa Silaha za Nyuklia Mashariki ya Kati mwaka 1995."
Afisa huyo amekumbusha kuwa, Israel inapaswa kuviweka vifaa vyake vyote vya nyuklia chini ya mfumo wa usimamizi wa IAEA na kujiunga na NPT na kuongeza kuwa hilo "ni sharti la kuanzisha eneo lisilo na silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati."

Kituo cha nyuklia za Dimona cha utawala haramu wa Israel

"Alisisitiza kuwa kukabiliana na kuenea kwa silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati ni msingi wa kazi zilizopewa IAEA."

Utawala haramu wa Israel, unafuata sera ya kimakusudi ya kutoweka wazi kadhia ya silaha zake za nyuklia. Inakadiriwa Israel ina vichwa vya nyuklia 200 hadi 400 katika ghala lake la silaha na kuifanya kuwa mmiliki pekee wa silaha za maangamizi eneo la Magharibi mwa Asia.
Utawala, hata hivyo, umekataa kuruhusu ukaguzi wa vituo vyake vya kijeshi vya nyuklia au kutia saini NPT.

Tags