Oct 06, 2023 02:47 UTC
  • Ansarullah yaionya Imarati kutokana na hatua inazochukua ndani ya Yemen

Mjumbe wa baraza la kisiasa la harakati ya Ansarullah ameionya Imarati kuhusu hatua na harakati zake inazoendesha huko Yemen.

Saudi Arabia kwa uungaji mkono wa Marekani, Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) na nchi nyingine kadhaa, iliivamia kijeshi Yemen tangu mwezi Machi mwaka 2015 na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa nchi kavu, baharini na angani. Moto wa vita uliowashwa na Saudi Arabia na waitifaki wake nchini Yemen hadi sasa umesababisha vifo vya Wayemeni zaidi ya elfu kumi na sita, kujeruhiwa makumi ya maelfu, na mamilioni ya wengine kulazimika kuyahama makazi yao.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Ali Al-Qahoum, mjumbe wa baraza la kisiasa la Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X (wa zamani wa Twitter) siku ya Alkhamisi: Imarati inataka kuendeleza uhusiano na Wazayuni; na nchi ambayo ina historia nyeusi ya ulaji njama dhidi ya mataifa ya eneo isifikirie kuwa Sana'a haifahamu vitendo inavyofanya katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Yemen.

Ali al-Qahoum

Afisa huyo wa Yemen ameongeza kuwa: Kwanza kabisa, Imarati inapasa ijue kwamba haiko katika kiwango cha kujilinganisha na Yemen na wala haitaruhusiwa kuendeleza njama zake huko Yemen, na ijue kwamba njama zote hizo zitaangamizwa.

Al-Qahoum amesisitiza kuwa Yemen, pamoja na wananchi wake, viongozi, jeshi lake kubwa na sekta zake za kijeshi, ambazo zinazidi kuwa na nguvu kila uchao, inaweza kushinda njama zote za Imarati.

Mjumbe huyo wa baraza la kisiasa la Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema: Imarati itatimuliwa kutoka Yemen na mipango yake ya njama na ya Kizayuni itakomeshwa, na siku zijazo zitajaa mambo mbalimbali ya kumshtukiza na kumshangaza adui.

Tarehe 26 Septemba, Abdul Malik Badruddin al-Houthi, kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen alisema kuwa iwapo mazungumzo hayatakuwa na tija watatumia nyenzo zote za kisheria kukomesha uchokozi na uvamizi dhidi ya nchi hiyo.../
 

 

Tags