Apr 11, 2024 09:54 UTC
  • Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Imarati, Uturuki wajadiliana matukio ya Ghaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika mazungumzo yake ya simu na mawaziri wenzake wa Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Uturuki kwamba kuna udharura wa kukomeshwa haraka jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza.

Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema katika mazungumzo yake na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Imarati, Sheikh Abdullah bin Zayed bin Sultan Aal Nahyan kwamba kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina inabidi kukomeshwe mara moja. Mawaziri hao wawili wamejadiliana pia masuala mengine ya kieneo na kimataifa katika mazungumzo yao hayo.

Vile vile Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo ya simu na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Uturuki, Hakan Fidan, na kutilia mkazo wajibu wa kuchukuliwa hatua za kivitendo za kuilazimisha Israel ikomeshe jinai zake dhidi ya Wapalestina. Mawaziri hao wawili wamejadiliana pia njia za kustawisha zaidi na zaidi ushirikiano wa Tehran na Ankara. 

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Uturuki

 

Mwaziri wa mambo ya Nje wa Iran na Uturuki wamejadiliana pia namna utawala wa Kizayuni unavyofanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza bila ya kisisi wala kuogopa chochote na vilevile matokeo mabaya ya mashambulizi ya Israel kwenye ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus, Syria.

Hossein Amir-Abdollahian ametumia pia fursa hiyo kutoa mwito wa kutumiwa vizuri sikukuu ya Idul Fitr kwa ajili ya kuimarisha umoja na mshikamano katika safu za Waislamu na kuimarisha amani kote ulimwenguni.

Tags