Apr 30, 2024 02:44 UTC
  • Kuharibiwa Gaza; Jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya kizazi cha sasa na kijacho

Mwezi wa saba wa vita unamalizika tangu utawala wa Kizayuni uanzishe vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza, huku mashambulizi ya kila siku ya utawala huo yakisababisha maafa na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya mji na afya katika ukanda huo.

Vita hivyo vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni Oktoba 7 mwaka jana dhidi ya Ukanda wa Gaza, mbali na kusabisha mauaji ya  kimbari katika Ukanda huo vimesababisha pia uharibifu mkubwa wa miundombinu muhimu ya maisha katika eneo hilo na kuifanya Gaza kuwa magofu.

Katika hujuma zake hizo za kikatili dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza, utawala wa Kizayuni unazishambulia nyumba za raia, skuli, misikiti, makanisa, kambi za wakimbizi na hospitali. Umoja wa Mataifa umetangaza baada ya kukamilisha tathmini iliyofanywa huko Gaza kwamba: Kumejiri uharibifu mkubwa katika mji wa Khan-Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza ambapo wawakilishi wa timu ya Umoja wa Mataifa waligundua kuwa kila jengo walilotembelea lilikuwa limebomolewa. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) pia limetangaza kuwa: Baada ya kupita zaidi ya siku 200 za vita dhidi ya Gaza, uharibifu mkubwa umefanywa kwa miundombinu muhimu katika eneo hilo. Uharibifu huo umetajwa kuwa mkubwa sana kuwahi kushuhudiwa katika historia. Wakati huo huo hasara na maafa yaliyosababishwa kwa miundomsingi muhimu ya Gaza pia ni nyingi sana, ambapo zaidi ya watu milioni moja wamepoteza makazi yao kikamilifu huku asilimia 75 ya wakazi wa eneo hilo wakilazimika kuyahama makazi yao.  

Wakazi wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza wamelazimika kuhama makazi yao kutoka na mauaji ya kimbari ya Israel 

Ripoti ya pamoja iliyochapishwa hivi majuzi na Benki ya Dunia na Umoja wa Mataifa ilitathmini uharibifu uliosababishwa kwa majengo na miundombinu muhimu huko Gaza kufuatia uvamizi wa Israel katika eneo hilo na kukadiria hasara hizo katika miezi 4 tu ya kwanza ya vita kuwa ni dola bilioni 18.5, ambayo ni sawa na asilimia 97 ya jumla ya pato la ndani la Gaza na Ukingo wa Magharibi mwaka 2022. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, maafa na hasara zilizosababishwa kwa miundombinu zimeathiri sekta zote za kiuchumi, na uharibifu uliosababishwa kwa makazi ya raia wa Gaza ni wa asilimia 72. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, karibu asilimia 19 ya uharibifu umetekelezwa kwa miundombinu ya huduma za jamii kama vyanzo maji, huduma za afya na elimu huku uharibifu wa asilimia 9 pia ukiripotiwa katika majengo ya biashara na elimu. 

Wakati huo huo asilimia 84 ya hospitali na vituo vya afya vya Gaza vimeharibiwa au kubomolewa; na vingine havifanyi kazi ipasavyo kutokana na ukosefu wa umeme au maji. Mfumo wa maji na maji taka huko Gaza unakaribia kusambaratika na unaweza kutoa asilimia 5 tu ya huduma zake za hapo awali.  

Hospitali ya al Shifa huko Gaza ilibomolewa katika mashambulizi ya Israel 

Kwa kuzingatia kiwango cha uharibifu na maafa yaliyosababishwa na vita vya utawala wa Kizayuni kwa miundombinu ya gaza;  Pierre Ludamar Afisa Mkuu wa Kitengo cha Kutegua Mabomu cha  Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa: Operesheni ya kuondoa vifusi huko Gaza kufuatia vita vya Israel dhidi ya eneo hilo huenda ikachukua takriban miaka 14. Jinai hizi zitaathiri pia maisha na kizazi cha sasa na maisha ya vizazi vijavyo vya wakazi wa Ukanda wa Gaza kutokana na madhara na maafa yaliyosababishwa na vita dhidi ya eneo hilo.