Dec 02, 2023 10:39 UTC
  • Hizbullah: Muqawama hautoruhusu Wazayuni wafikie malengo yao Ghaza

Naibu wa Mkuu wa Baraza la Utendaji la Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amegusia kuanza upya jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza na kusema kuwa, muqawama kamwe hautowaruhusu Wazayuni kufanikisha malengo yao haramu.

Utawala wa Kizayuni wa Israel jana Ijumaa ulianzisha wimbi jipya la jinai na mashambulizi yake dhidi ya wananchi wa Ghaza baada ya kukwamisha kwa makusudi mazungumzo ya kusimamisha vita.

Shirika la habari la Tasnim limemnukuu Sheikh Ali Da'mush, Naibu wa Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon akisema hayo na kuongeza kuwa, utawala wa Kizayuni umeanzisha mashambulio na jinai mpya dhidi ya Ukanda wa Ghaza kwa kibali na idhini kamili ya Marekani na kwamba walimwengu wameshajua ukweli halisi kuhusu kadhia ya Palestina na hivyo hila na uongo wa Marekani hauwezi kuficha tena uhakika wa mambo.

Sheikh Ali Da'mush

 

Amesema, tangu mwanzo kabisa vita vya Ghaza vilikuwa ni vita vya Marekani dhidi ya wananchi wanaodhulumiwa kiila upande wa Palestina na hilo linathibitishwa na kila kipengee cha vita hivyo tangu kuanza kwake tarehe 7 Oktoba, hadi kusitishwa kwa muda na mpaka hivi sasa ambapo utawala wa Kizayuni umeanzisha wimbi jipya la jinai dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Ghaza.

Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Hizbullahi ya Lebanon ameongeza kuwa, njama za Marekani za kujaribu kusafisha sura yake mbele ya fikra za walio wengi duniani kupitia kujifanya inapenda amani, haziwezi kuficha ukweli wa kushiriki kwake kikamilifu katika mauaji ya watoto wachanga na raia wasio na hatia huko Ghaza, na hakuna yeyote anayeweza kuhadaiwa na njama hizo.

Amesema, adui Mzayuni anapaswa kuelewa kuwa, imani na ari ya muqawama ni madhubuti na kubwa sana na kwamba jinai za adui huyo dhidi ya wananchi wa Ghaza haziwezi kufifiliza kipigo ilichopata Israel kutoka kwa wanamapambano wa Palestina kupitia operesheni ya #Kimbunga_cha_al-Aqsa.

Tags