Dec 03, 2023 10:43 UTC
  • Askari 60 wa Kizayuni waangamizwa katika operesheni ya HAMAS

Makumi ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wameangamizwa katika operesheni ya Brigedi za Izzuddin al Qassam, Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu HAMAS.

Izzuddin al Qassam imesema katika taarifa leo Jumapili kuwa, wanamapambano wake wameshambulia kambi ya wanajeshi wa Israel katika kijiji cha Juhor ad-Dik, kusini mwa jiji la Gaza, ambapo askari wasiopungua 60 wa Kizayuni wameangamizwa.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, wanajihadi wa Brigedi za Izzuddin al Qassam, Tawi la Kijeshi la Harakati ya HAMAS wamefanikiwa kutega mabomu na mada za miripuko pambizoni mwa kambi hiyo, na kisha kuziripua zote kwa wakati mmoja.

Qassam imeongeza kuwa, baada ya kufanya operesheni hiyo iliyowasababishia Wazayuni hasara kubwa za roho na mali, wapiganaji hao wa HAMAS wamefanikiwa kuondoka salama bila kujeruhiwa.

Jeshi la utawala haramu wa Israel limethibitisha habari ya kujiri operesheni hiyo kusini mwa Gaza, ingawaje linadai kuwa askari wake waliouawa katika operesheni hiyo ni wawili tu. 

Mwanajihadi wa Izzuddin al Qassam

Jana jioni, Brigedi za Izzuddin al Qassam zilitangaza kwamba zimeendelea kuipiga kwa makombora miji ya utawala wa Kizayuni ukiwemo mji mkuu Tel Aviv ili kujibu jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

HAMAS imesema wazi kwamba hakuna mabadilishano yoyote ya mateka yatakayofanyika ila baada ya utawala wa Kizayuni kukomesha kikamilifu jinai zake dhidi ya wananchi wa Gaza.

Utawala dhalimu wa Israel ambao umeshindwa kwenye medani za mapambano, umeamua kumalizia hamaki zake kwa kuua watoto wadogo, wanawake, vizee na raia wa kawaida huko Gaza.

Kwa mujibu Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, tangu kuanza kwa mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7, Wapalestina zaidi ya 15,207 wameuawa shahidi, na kwamba idadi ya waliojeruhiwa imepindukia watu 40,652.

Tags