Mar 03, 2024 07:39 UTC
  • Wanajihadi wa HAMAS wadhibiti ndege isiyo na rubani ya Israel

Wanamapambano wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS wametangaza habari ya kutwaa na kudhibiti ndege isiyo na rubani ya Israel (droni), ikiwa ni kuendelea kujibu jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

IRNA imenukuu shirika la habari la Shihab lililoripoti kuwa, wanajihadi wa Brigedi za Izzuddin al-Qassam, tawi la kijeshi la HAMAS walitwaa droni hiyo ya Israel aina ya SkyLark UAV jana Jumamosi, ilipokuwa ikiruka katika anga ya kijiji cha Al-Zaytoun, viungani mwa jiji la Gaza.

Taarifa ya Brigedi za Izzuddin al-Qassam imeleeza bayana kuwa, ndege hiyo isiyo na rubani ya Israel iliyotwaliwa ilikuwa ikifanya ujasusi katika Ukanda wa Gaza.

Makundi ya muqawama ya Palestina, Lebanon na Yemen mara kadhaa yamefanikiwa kukamata droni za kijasusi za utawala wa Kizayuni zikiruka katika anga za nchi hizo za Asia Magharibi.

Katika hatua nyingine, Brigedi za Izzuddin al-Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema muqawama tu ndio utakaoamua kuhusu hatima na mustakabali wa Ukanda wa Gaza.

Abu Hamza, msemaji wa Qassam

Abu Hamza, msemaji wa Qassam amemuonya vikali Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel juu ya kile kinachoitwa mpango wa baada ya vita wa utawala huo pandikizi na kueleza kuwa, "Ujumbe wetu kwa adui na kiongozi wa kumbo, Netanyahu upo wazi, kwamba suala la 'siku baada ya mpango' huko Gaza litaamuliwa tu na muqawama wa Palestina."

Hivi karibuni pia, Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS alisema harakati hiyo imekuwa ikionesha nia ya kutaka makubaliano ya kusimamisha vita na Israel lakini hiyo haina maana kuwa haiko tayari kuendelea na mapambano dhidi ya utawala huo dhalimu.

Tags