Apr 19, 2024 10:23 UTC
  • Waziri wa Israel: Mashambulizi ya Iran yameharibu kambi mbili kuu za jeshi; akejeli taarifa za Israel kushambulia Iran + Video

Waziri wa Usalama wa Ndani ya serikali ya Benjamin Netayahu amekiri kwamba shambulio la kulipiza kisasi la Iran dhidi ya Israel limesababisha hasara kubwa za kijeshi kwa utawala wa Kizayuni na wakati huo huo ameziita taarifa zilizodai kuwa utawala wa Kizayuni umefanya shambulizi ndani ya Iran leo Ijumaa kuwa ni istihzai.

Mkanda wa video ulioenea kwenye mitandao ya kijamii unamuonesha waziri wa usalama wa ndani wa utawala wa Kizayuni, Itamar Ben-Gvir akikiri kwamba tangu tarehe 7 Oktoba 2023 hadi hivi sasa, shambulio la kulipiza kisasi la Iran ndilo shambulio kubwa zaidi kufanyika dhidi ya utawala wa Kizayuni. Anasikika akisema: Israel imekumbwa na shambulio kubwa ambapo kambi zake mbili kuu za jeshi la anga zimepigwa na kuteketezwa.

Mkanda huo wa video hauoneshi umerekodiwa lini lakini umesambazwa na vyombo mbalimbali vya lugha ya Kiarabu ikiwemo Russia Today. Ndani ya video hiyo, waziri huyo wa usalama wa ndani wa utawala wa Kizayuni  hakuzitaja kwa majina kambi hizo za kijeshi za Israel zilizoangamizwa kwenye mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran. Lakini Kamanda wa Komandi Kuu ya Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Baqeri alisema mara baada ya Jamhuri ya Kiislamu kuitia adabu Israel kwamba kambi ya Nevatim ya jeshi la anga la utawala wa Kizayuni ilikuwa ni moja ya shabaha kuu za mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran. 

 

Amma kuhusiana na habari zilizoenea leo Ijumaa kuhusu utawala wa Kizayuni kufanya shambulio nchini Iran, waziri wa usalama wa ndani wa Israel amekejeli taarifa hizo na kusema ni istihzai.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Itamar Ben Gvir ameonesha hisia zake kuhusu habari hiyo kwa kuandika neno moja tu kwenye mtandao wa kijamii wa X linalosema: "Ni istihzai."

Vyombo vya habari vya Magharibi, mapema leo Ijumaa vimeeneza kwa wingi madai kuwa, utawala wa Kizayuni umeishambulia Iran baada ya kusikika sauti kali katika mkoa wa Isfahan wa katikati mwa Iran. Lakini imebainika kuwa, sauti hizo zimetokana na kutunguliwa videge vitatu vidogo visivyo na rubani vilivyoonekana kwenye anga ya mji huo kabla ya kufika popote.