Mar 05, 2021 13:20 UTC
  • Papa Francis awasili Baghdad, Iraq katika safari yake ya kihistoria

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amewasili Baghdad mji mkuu wa Iraq katika ziara yake ya kihistoria ya siku tatu katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani alilakiwa na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo akiwemo Waziri Mkuu Mustafa al-Kadhimi.

Katika safari yake hiyo, Papa Francis mbali na kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa Iraq, anatarajiwa pia kuwa na mazungumzo mjini Najaf na Ayatullah Ali Sistani, Marjaa wa Kishia na kiongozi mkubwa wa kidini nchini humo.

Aidha Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani anatarajiwa kuitembea pia miji ya Irbil, Mosul na Nasiriya.

Safari ya Papa Francis nchini Iraq inafanyika huku usalama ukiwa umeimarishwa mno sambamba na kuongezeka maambukizo ya virusi vya Corona.

Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani akiongozana na Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq mara baada ya kuwasili katikka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad (Ijumaa 05.03.2021)

 

Ikiwa hii ni safari yake ya kwanza ya nje tangu kulipoibuka virusi vya Corona, Kiongozi wa Kanisa Katioliki Duniani anatarajiwa kuwasilisha risala ya mshikamano sio baina ya Wakristo tu bali baina ya wananchi wote wa Iraq.

Kabla ya kuelekea Iraq, Papa Francis alitoa ujumbe kupitia mkanda wa video akisema kuwa, anaelekea nchini humo kama mfanyaziara aliyebeba ujumbe wa amani na anafutilia suala la udugu na maridhiano baina ya Wairaq.

Safari hii inahesabiwa kuwa ni ya kihistoria hasa kwa kutilia maanani kwamba, ni mara ya kwanza katika historia kwa Papa kuitembelea Iraq.

Tags