Apr 25, 2021 09:31 UTC
  • Rais Barham Salih wa Iraq aamuru uchunguzi mlipuko wa hospitali ya wagonjwa wa corona, makumi wamefariki dunia

Rais Barham Salih wa Iraq ametoa amri ya kufanyika uchunguzi kuhusiana na mlipuko uliotokea mapema leo katika Hospitali ya Ibn Khatib mjini Baghdad iliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa corona. Makumi ya wagonjwa wameuawa katika ajali hiyo.

Agizo hilo la Rais wa Iraq limetolewa baada ya serikali kutangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kwa heshima ya wahanga wa ajali hiyo.

Ripoti zinasema kuwa watu wasiopungua 82 wameaga dunia hadi sasa na makumi ya wengine wamejeruhiwa katika ajali hiyo iliyosababishwa na kuripuka mitungi ya oksijeni. 

Taarifa iliyotolewa na Rais wa Iraq imetaka kufanyike uchunguzi na kuhojiwa wale wote wanaodhaniwa kuzembea na kusababisha ajali hiyo. Vilevile Rais wa Iraq ametoa agizo la kutumiwa suhula zote za lazima kwa ajili ya kuwasaidia majeruhi na waathirika wa mlipuko huo. Tayari maafisa wawili wametiwa nguvuni kuhusiana na ajali hiyo. 

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iraq, moto huo umetokea kwenye hospitali ya Ibn Khatib katika eneo la Jisr Diyala, mjini Baghdad. Ripoti zinaeleza kuwa, wagonjwa zaidi ya 82 wa corona wamefariki dunia na makumi ya wengine wamejeruhiwa kutokana na msongo wa pumzi.

Kikosi cha zima moto kikiokoa maisha ya wagonjwa wa corona, Baghdad

Mkurugenzi wa Ulinzi wa Miji nchini Iraq amesema kuhusiana na ajali hiyo kwamba, hospitali hiyo ilikuwa na wagonjwa 120 wa virusi vya corona.

Kadhim Souhan amesema, moto huo umetokea katika ghorofa ya kati ya hospitali hiyo ya Ibn Khatib. Ameongeza kuwa, kutokea kwa moto huo kumepelekea kukatika kwa oksijini wanayopatiwa wagonjwa wa corona na kuifanya hali iwe ngumu zaidi kwa wagonjwa hao.

Tags