Dec 18, 2021 12:49 UTC
  • Palestina yataka jamii ya kimataifa izuie ugaidi wa Israel

Wizara ya Mambo ya Nje ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura za kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel usitishe vitendo vya kigaidi vinavyotekelezwa na walowezi wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, achukue hatua za haraka za kutumia mfumo wa kimataifa kuwalinda Wapalestina wanaokabiliwa na ugaidi wa utawala ghasibu wa Israel.

Imesema kuna wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la hujuma zilizoratibiwa za walowezi wa Kizayuni hasa katika vijiji vya Ukingo wa Magharibi vya Qaryout na Burqa na pia mtaa wa Sheikh Jarrah katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Quds Mashariki (Jerusalem).

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imesema, Waziri Mkuu wa Utawala wa Israel mwenye misimamo mikali, Naftali Bennet anabeba dhima ya hujuma na ugaidi wa walowezi wa Kizayuni na kuonya kuwa vitendo hivyo vitakuwa na matokeo mabaya kwa eneo zima la Magharibi mwa Asia.

Vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina

Zaidi walowezi wa Kizayuni laki sita wanaishi katika vitongoji 230  ambavyo ni kati ya ardhi za Palestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambazo zilivamiwa na utawala haramu wa Israel mwaka 1967. Vitongoji vyote hivyo vimejengwa kinyume cha sheria za kimataifa, na Umoja wa Mataifa umelaani vikali ujenzi wa vitonogji hivyo.

Utawala wa Kizayuni unaendeleza ujenzi huo haramu wa vitongoji katika ardhi za Palestina huku ukipuuza takwa la jamii ya kimataifa la kusimamisha ujenzi huo kwa kukingiwa kifua na Marekani. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ujenzi wa vitongoji vyote vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na Israel katika ardhi za Palestina ni kinyume cha sheria.  

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, hadi sasa utawala wa Israel haujachukua hatua yoyote ya kutekeleza azimio nambari 2234 la tarehe 23 Disemba 2016 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. 

Tags