Oct 16, 2022 10:44 UTC
  • Makumi ya magaidi wa ISIS wauawa katika operesheni ya jeshi la Syria

Makumi ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) wameangamizwa katika operesheni ya jeshi la Syria kusini mwa nchi.

Duru za kiusalama zimeliambia shirika rasmi la habari la Syria SANA kuwa, idadi kubwa ya magaidi wa ISIS wameuawa katika operesheni ya jeshi la Syria likishirikiana na makundi ya kujitolea wananchi katika mkoa wa Dara'a, kusini mwa nchi.

Habari zaidi zinasema kuwa, magaidi wengine wengi wa genge hilo la ukufurishaji wamejeruhiwa vibaya kwenye operesheni hiyo inayoonekana kuwa ya ulipizaji kisasi ya vyombo vya ulinzi na usalama vya Syria.

Haya yanajiri siku chache baada ya makumi ya wanajeshi wa Syria kuuawa katika shambulio la bomu lililolenga basi la maafisa na askari wa jeshi la nchi hiyo ya Kiarabu.

Syria kwa miaka mingi imekuwa ikilalamikia uwepo haramu wa kijeshi wa Marekani nchini humo

Duru za habari zilialiambia shirika rasmi la habari la Syria SANA kuwa, hujuma hiyo ya kigaidi ilitokea Alkhamisi iliyopita viungani mwa mji mkuu Damascus kusini magharibi mwa nchi, ambapo wanajeshi 27 wa Syria walijeruhiwa pia kwenye tukio hilo. 

Hivi karibuni, shirika la habari la SANA likinukuu vyanzo vya ndani vilivyozungumza kwa sharti la kutotajwa jina liliripoti kwamba, mabaki ya magaidi wa Daesh wanapewa mafunzo katika kambi ya Jeshi la Marekani katika mji wa al-Shaddadi wa mkoa wa Hasakah, kaskazini mashariki mwa Syria. 

Serikali ya Damascus kwa miaka mingi sasa imekuwa ikilalamikia uwepo haramu wa kijeshi wa Marekani nchini Syria.

Tags