Dec 28, 2022 04:20 UTC
  • Wizara ya Afya ya Yemen: Uvamizi na mzingiro umesababisha magonjwa ya kuambukiza

Msemaji wa Wizara ya Afya ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema hatua ya muungano vamizi wa Saudi Arabia ya kutekeleza hujuma za kikatili na mzingiro wa ukandamizaji dhidi ya watu wa Yemen imesababisha kuenea magonjwa mbalimbali ya kuambukiza nchini humo.

Saudi Arabia ikiungwa mkono na kushirikiana na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na nchi nyingine kadhaa mwezi Machi 2015 zilianzisha hujuma ya kijeshi huko Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa baharini, anga na nchi kavu. 

Mzingiro wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen umeathiri pakubwa sekta ya afya ya nchi hiyo na kusababisha vituo vya afya na hospitali za nchi hiyo kukosa dawa na vifaaa vya tiba.  

Televisheni ya al Masira imeripoti kuwa, Najib al Qabati Msemaji wa Wizara ya Afya ya Yemen ametangaza kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia unazishambulia hospitali, zahanati na vituo vya afya vya kudhibti magonjwa ya kuambukiza huku ukizuia kuingizwa dawa nchini humo. 

Hujuma za Saudia kwa hospitali na vituo vya afya, Yemen 

Al Qabati ameongeza kuwa, hujuma za nchi vamizi mbali na kuwalenga wafanyakazi wa sekta ya tiba na wa huduma za afya za dharura zimeviathiri pia vituo vya kudhibiti ugonjwa wa malaria na kutoa huduma kwa wagonjwa wa kipindupindu. Amesema, maji machafu ni moja ya sababu kuu za  kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza nchini Yemen, ambapo wananchi katika baadhi ya maeneo wanatumia maji machafu kutokana na kuhujumiwa miundo mbinu ya maji safi ya kunywa.  

Tags