Feb 10, 2023 02:26 UTC
  • Duru mpya ya mazungumzo baina ya Iran na Saudia kufanyika hivi karibuni Baghdad, Iraq

Waziri Mkuu wa Iraq ametangaza kuwa duru mpya ya mazungumzo kati ya Iran na Saudi Arabia itafanyika hivi karibuni mjini Baghdad.

Tarehe 3 Januari 2016, Saudi Arabia ilivunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran kwa kisingizio cha baadhi ya watu kushambulia ubalozi wake mjini Tehran na ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Mashhad.
Hadi sasa, duru tano za mazungumzo kati ya Iran na Saudi Arabia zimefanyika katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.
Katika duru ya tano ya mazungumzo kati ya wawakilishi wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia mjini Baghdad, mwanga mkubwa zaidi wa matarajio ulijitokeza kwa ajili ya kurejeshwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Waziri Mkuu wa Iraq Mohammad Shia al-Sudani

Katika mahojiano na gazeti la Al-Sharq Al-Awsat, na wakati akijibu suali aliloulizwa kuhusu duru mpya ya mazungumzo kati ya Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammad Shia al-Sudani, amesema, duru mpya ya mazungumzo hayo itafanyika hivi karibuni, na kwamba tangu serikali mpya ya Iraq ilipoanza kazi rasmi, imekuwa ikifanya juhudi kulingana na ombi la Tehran na Riyadh za kuendeleza uhusiano kati ya pande hizo mbili.

Al-Sudani ameongeza kuwa, Iraq inauona uhusiano huo kuwa ni wenye umuhimu, kwa sababu kadiri maoni na mitazamo tofauti iliyopo katika eneo hili inavyokaribiana, ndivyo utulivu zaidi utakavyopatikana.
Waziri Mkuu wa Iraq amesisitiza kuwa, Baghdad inaendelea kutoa mchango wake wa upatanishi katika mazungumzo hayo, na akasema, ana matumaini kuwa vikao vya ngazi ya usalama vilivyofanyika kati ya Tehran na Riyadh vitapandishwa hadi ngazi ya kidiplomasia, na kwamba lengo la Iraq ni kuinua kiwango hicho cha mikutano ya maafisa wa usalama kufikia ngazi ya mahusiano ya kidiplomasia.
Al-Sudani aidha amesema, "mimi binafsi nitashiriki katika mikutano hiyo na kulifuatilia suala hilo".../

 

Tags