May 27, 2023 10:49 UTC
  • Saudia yatoa miongozo kwa mahujaji, imo marufuku ya kupiga picha maeneo matakatifu

Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia imetoa taarifa ya miongozo kwa mahujaji wa mwaka huu wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu.

Ibada ya Hija ndio mkusanyiko mkubwa zaidi wa Waislamu, ambao hufanyika kila mwaka katika mwezi wa Dhul-Hijjah katika mji mtakatifu wa Makka na kandokando yake nchini Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Al-Wat'an, katika taarifa yake hiyo, Wizara ya Hija na Umra ya Saudia imesema, ili kurahisisha masuala ya kiidara yanayohusiana na safari, mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu wabebe hati zao rasmi hasa zinazohusiana na amali za Hija na kuchukua mizigo mepesi wakati wa utekelezaji wa amali za Hija.
Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia imetangaza kuwa mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu hawaruhusiwi kuchapisha au kusambaza tarifa za habari bila idhini ya Wizara ya Habari. Aidha wajiepushe kufanya mikusanyiko yenye malengo ya kisiasa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia, ni marufuku kuweka mikusanyiko kwa ajili ya usomaji dua kwa pamoja, kupaza sauti au kutekeleza ibada za kidini katika Haram mbili Tukufu za Makka na Madina.
Kwa mujibu wa miongozo hiyo, mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu wametakiwa wazingatie pia kwamba ni marufuku kuchukua filamu na kupiga picha ndani ya maeneo matakatifu.
Inakadiriwa kuwa mwaka huu, Saudi Arabia itapokea mahujaji zaidi ya milioni mbili, kiasi kwamba mashirika ya ndege ya nchi hiyo yameshatenga tiketi zaidi ya 1,200,000 kwa ajili ya wageni wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu. Viwanja sita vya ndege vya ndani ikiwa ni pamoja na Jeddah, Riyadh, Al-Dammam, Madinatul-Munawwara, Al-Taif na Yan'ba vitapokea ndege zitakazobeba mahujaji wa mwaka huu.../

 

Tags