May 18, 2023 09:20 UTC
  • Umuhimu wa kisiasa wa ibada ya Hija katika maneno ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei asubuhi ya jana Jumatano (tarehe 17 Mei) alieleza baadhi ya vipengee umuhimu vya kisiasa vya ibada ya Hija katika kikao chake na maafisa, wasimamizi na baadhi ya Wairani waliojiandikisha kushiriki ibada ya Hija mwaka huu.

Hija ni mojawapo ya faradhi za Kiislamu ambazo, pamoja na faida zake za kidini, pia ina vipengee muhimu vya kisiasa. Kiongozi wa Mapinduzi Kiislamu daima amekuwa akisisitiza faida za kisiasa za ibada hiyo ya Hija sambamba na vipengee vyake vya kidini. Katika hotuba yake ya jana pia Ayatullah Khamenei aliashiria baadhi ya vifungu muhimu vya kisiasa vya ibada hiyo. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi katika mkutano kuhusu Hija

Kwanza ni kwamba, ibada ya Hija huyakurubisha zaidi mataifa ya Kiislamu. Moja ya stratijia muhimu za madola ya Magharibi hasa Marekani, kuhusiana na Ulimwengu wa Kiislamu ni kuzusha hitilafu baina ya nchi za Kiislamu. Kwa kuwa watu kutoka nchi mbalimbali huelekea Saudi Arabia katika msimu wa Hija, suala hilo hutayarisha fursa ya mazungumzo baina ya mataifa ya Kiislamu, kubadilisha mitazamo na kuchukua hatua za kubatilisha stratijia ya nchi za Magharibi. Kuhusiana na suala hilo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Hija ni suala la kimataifa na la kiustaarabu ambalo lengo lake ni kustawisha Umma wa Kiislamu, kuzikurubisha zaidi nyoyo za Waislamu na kuunganisha Umma wa Kiislamu dhidi ya ukafiri, dhulma, ubeberu na masanamu ya kibinadamu na yasiyo ya kibinadamu."

Pili ni kwamba, miongoni mwa vipengee muhimu vya  kisiasa ya ibada ya Hija, ambavyo vimesisitizwa katika hotuba ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ni mtazamo aali wa Uislamu kuhusiana na haki za binadamu. Katika upande mmoja, nchi za Magharibi zinadai kuwa juu na bora zaidi katika kanuni za haki za binadamu, na kwa upande mwingine, zinazituhumu nchi nyingine hasa za Kiislamu kuwa zinakiuka haki za binadamu. Wamagharibi pia wana mtazamo wa kinafiki na kindumakuwili kuhusiana na haki za binadamu. Kwa mfano tu wakati wanasadia ukiukaji wa haki za binadamu nchini Yemen, Wamagharibi tunawaona wakitia chumvi madai ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Ukraine.

Msimu wa Hijja ni fursa ambayo inabatilisha madai ya Wamagharibi kuhusiana na haki za binadamu na kudhihirisha utukufu wa mwanadamu bila kujali rangi, mbari, tabaka wala jiografia. Kuhusiana na hili, Ayatullah Khamenei amesema Uislamu umepinga kivitendo ubaguzi unaotegemea masuala ya kijiografia, rangi, mbari, tabaka na tofauti nyinginezo kupitiai ibada ya Hija na kuongeza kuwa: Nchi zinazodai kustaarabika, kwa hakika hazijanusa hata harufu ya ustaarabu, na zingali zinashughulishwa na kadhia ya watu weusi na weupe, na wazungu na wasio wazungu; na zinathamini zaidi wanyama wao wa ndani kuliko binaadamu wengine, na hapana shaka kuwa kuzama mara kwa mara wahamiaji baharini kunakopuuzwa na nchi za Magharibi ni uthibitisho wa ukweli huu. Mafundisho ya Uislamu ya kuondoa ubaguzi yanashuhudiwa kivitendo katika ibada ya Hija ambapo watu weusi kwa weupe kutoka kila pembe ya dunia na kutoka staarabu tofauti, wote wanajumuika pamoja bila ya kubaguana."

Ayatullah Khamenei akizungumza na maafisa, wasimamizi na baadhi ya Wairani waliojiandikisha kushiriki ibada ya Hija mwaka huu. 

Kipengele cha tatu muhimu cha kisiasa cha ibada ya Hija ni uungaji mkono kwa Palestina na kuchukizwa na utawala ghasibu wa Kizayuni. Msimu wa Hija ni moja ya fursa zinazotumiwa kutoa nara za kuunga mkono Palestina na kulaani jinai za Israel katika jamii ya Waislamu. Pia, wakati wa msimu wa Hija, kunaelezwa upinzani dhidi ya ubeberu na kauli mbiu za kupinga Marekani. Kuhusiana na suala hilo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja umoja wa Umma wa Kiislamu na kukabiliana na mashetani wenye kiburi na mabeberu kuwa ni miongoni mwa malengo muhimu ya ibada ya Hija na kuongeza kuwa: Miongoni mwa manufaa mengi ya duniani ya Hija ni kwamba katika mkusanyiko huo mkubwa, Waislamu wanatangaza uwepo na nguvu zao mbele ya utawala wa Kizayuni na ushawishi wa madola ya kibeberu, na wanasimama kidete dhidi ya madhalimu wa dunia.

Jambo la mwisho ni kwamba, kutokana na vifungu hivi muhimu vya Hija vya kuimarisha umoja, kuzindua umma na kupambana na maadui, baadhi ya madola ya Magharibi na utawala wa Kizayuni wa Israel yana mtazamo hasi kuhusu Hija na yanaiwekea mashinikizo serikali ya Saudi Arabia ili izuie baadhi ya vipengee muhimu vya ibada hiyo hasa "amali ya kujibari na kujitenga na washirikina."

Tags