Mar 20, 2024 15:01 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Muqawama umevunja njama za Marekani katika eneo

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongeza operesheni za makundi ya muqawama ya Palestina, Yemen, Syria, Iraq, na Lebanon dhidi ya utawala wa Kizayuni na kusisitiza kuwa, mrengo wa mapambano ya Kiislamu umefanikiwa kusambaratisha njama za Marekani katika eneo la Asia Magharibi.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumatano hapa Tehran katika hotuba yake kwa taifa, kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa Kiirani wa 1403 Hijria Shamsia na kuongeza kuwa, "Kambi ya Muqawama imedhihirisha uwezo wake, na kwa mafanikio makubwa imeweza kuvuruga mahesabu ya kistratejia ya Washington Asia Magharibi."

Amesema ndoto ya muda mrefu ya Marekani ya kulitawala na kulidhibiti eneo hili imesambaratishwa na ukakamavu wa mrengo wa muqawama, na chaguo ililonalo Washington hivi sasa ni kufungasha virago na kuondoka katika eneo.

Ayatullah Ali Khamemeni amepuuzilia mbali madai ya Wamagharibi kwamba Iran ndiyo inayafanyia maamuzi makundi ya muqawama katika eneo na kubainisha wazi kuwa, pamoja na kwamba Jamhuri ya Kiislamu inaziunga mkono harakati za mapambano katika eneo, lakini harakati hizo zinajichukulia maamuzi zenyewe. 

Kiongozi Muadhamu ameashiria masaibu na madhila wanayokumbana nayo Wapalestina na kubainisha kuwa, "Hakuna mtu yeyote mwenye hisia za utu atanyamazia kimya dhulma na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza."

Kiongozi Muadhamu

Amesisitiza kuwa, Marekani ndiyo iliyopata hasara na ndiye mshindwa mkubwa katika vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza.  "Uungaji mkono usio na kifani wa Washington kwa Israel umetia doa kwenye hadhi ya Marekani duniani, na kuchochea mara kumi hisia za chuki dhidi ya Washington katika eneo," ameongeza Kiongozi Muadhamu. 

Awali Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alitoa ujumbe muhimu kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa Kiirani wa 1403 Hijria Shamsia na ameuita mwaka huo kuwa ni wa mapinduzi ya kiuchumi kwa kushirikisha wananchi.

Tags