Jun 01, 2024 10:24 UTC
  • Barua ya Kiongozi Muadhamu kwa wanachuo wa Marekani

Ifuatayo ni barua ya Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, aliyowaandikia wanachuo wa vyuo vikuu vya Marekani kufuatia utetezi wao wa kijasiri kwa maslahi ya watu wa Palestina.

Bismillahir Rahmanir Rahim (Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu)

Ninawaandikia barua hii vijana ambao dhamiri zao zilizo hai zimewasukuma kuwatetea watoto na wanawake wanaodhulumiwa wa Gaza.

Wapendwa wanachuo vijana wa Marekani! Huu ni ujumbe wetu wa mfungamano na mshikamano na nyinyi. Nyinyi hivi sasa mumesimama upande sahihi wa historia - ambayo kurasa zake zinaendelea kufunguka.

Sasa mmeunda sehemu ya mrengo wa Muqawama, ambapo mumeanzisha mapambano ya heshima na ya kijasiri, chini ya mashinikizo ya kikatili ya serikali yenu - ambayo inatetea wazi wazi utawala ghasibu na wa katili.

Mrengo mkubwa wa Muqawama katika eneo la mbali umekuwa ukipambana kwa miaka mingi ukiwa na ufahamu na hisia hizi hizi mlizonazo leo. Lengo la mapambano haya ni kukomesha dhulma ya wazi ambayo mtandao wa kigaidi na kikatili unaoitwa "Wazayuni" umekuwa ukilifanyia taifa la Palestina tangu miaka mingi nyuma, ambapo umewaweka chini ya mateso makali na mashinikizo makubwa baada ya kupora na kuikalia kwa mabavu nchi yao. Mauaji ya kimbari yanayotekelezwa leo na utawala wa kibaguzi wa Kizayuni ni mwendelezo wa tabia yake ya ukatili wa kupindukia, ya miongo kadhaa iliyopita.

Palestina ni nchi huru ya taifa linaloundwa na Waislamu, Wakristo na Wayahudi ambayo ina historia ndefu sana. Baada ya Vita vya Dunia, mabepari wa mtandao wa Kizayuni, wakisaidiwa na serikali ya Uingereza, hatua kwa hatua walituma magaidi elfu kadhaa katika ardhi hii; wakavamia miji na vijiji vyake, ambapo waliua kwa umati maelfu ya watu au kuwafukuza na kuwahamishia katika nchi jirani. Walipora na kunyakua nyumba, masoko, na mashamba yao, na wakaanzisha taifa linaloitwa Israeli katika ardhi iliyonyakuliwa ya Palestina.

Muungaji mkono mkuu wa utawala huu ghasibu, baada ya misaada ya kwanza ya Uingereza, ni serikali ya Marekani, ambayo imeendeleza uungaji mkono wake wa kisiasa, kiuchumi na silaha kwa utawala huo, na hata kufanya uzembe usiosameheka kwa kuufungulia njia ya kuzalisha silaha za nyuklia, na kuusaidia katika njia hiyo.

Tangu siku ya kwanza, utawala wa Kizayuni umetumia sera ya "Mkono wa Chuma" dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Palestina, ambapo umepuuza maadili yote ya dhamiri ya kibinadamu na ya kidini, na kuzidisha ukatili, ugaidi na ukandamizaji wake siku baada ya siku.

Serikali ya Marekani na washirika wake hata hawajaonyesha kuchukizwa hata kidogo na ugaidi huu unaodhaminiwa na serikali na dhulma inayoendelea. Leo pia, baadhi ya kauli zinazotolewa na serikali ya Marekani kuhusu jinai za kutisha huko Gaza, kabla ya kuwa ni za kweli ni unafiki mtupu.

Mrengo wa Muqawama ulidhihiri kutoka katika kitovu cha mazingira haya haya ya kiza na ukataji tamaa na kupelekea kuundwa kwa serikali ya "Jamhuri ya Kiislamu" nchini Iran ambayo imeeneza na kuupa nguvu mrengo huu.

Viongozi wa Uzayuni wa kimataifa, ambao wanamiliki mashirika mengi ya vyombo vya habari huko Marekani na Ulaya au wameviathiri kwa pesa na rushwa, wanautuhumu muqawama huu wa kibinadamu na wa kishujaa kuwa ni ugaidi! Je, taifa linalojitetea katika ardhi yake dhidi ya jinai za Wazayuni maghasibu wa Kizayuni ni magaidi? Na je, misaada ya kibinadamu kwa taifa hili na kuliimarisha ni kusaidia ugaidi?

Viongozi wa mfumo wa ubeberu unaotumia mabavu hawana hata huruma kwa thamani za kibinadamu. Wanadai kuwa utawala katili na wa kigaidi wa Israel unajilinda, na kuutuhumu muqawama wa Palestina unaotetea uhuru, usalama na haki yake ya kujitawala kuwa ni "ugaidi"!

Ninataka kukuhakikishieni kwamba leo hali inaendelea kubadilika. Hatima nyingine inalisubiri eneo nyeti la Asia Magharibi. Dhamiri nyingine nyingi zimeamka ulimwenguni kote na ukweli unaendelea kufichuka. Mrengo wa Muqawama umepata nguvu na bila shaka utapata nguvu zaidi. Historia pia inaendelea kubadilika.

Mbali na nyinyi wanachuo wa makumi ya vyuo vikuu vya Marekani, vyuo vikuu na watu wa nchi nyingine pia wanapambana. Ushirikiano na uungaji mkono wa wahadhiri wa vyuo vikuu kwenu wanachuo ni tukio muhimu na lenye taathira. Hili linaweza kukufarijini kwa kiasi fulani kwa kupunguza makali ya ukandamizaji wa polisi na mashinikizo yanayotolewa dhidi yenu. Mimi pia ninashikamana na ninyi vijana na kuheshimu mapambano yenu.

Qur’ani inatufundisha sisi Waislamu na watu wote duniani kusimama imara na kupambana katika njia ya haki: "Msidhulumu wala msidhulumiwe." Kwa kufuata amri hii na mamia ya amri nyingine zinazofanana nayo, bila shaka Muqawama utasonga mbele na kupata ushindi; Mungu akipenda.

 

Ninakunasihini mpate kusoma na kuijua Qur'an.

Seyyed Ali Khamenei

25/05/2024

 

Tags