Umoja wa Afrika watoa wito wa kusitishwa vita nchini DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136474-umoja_wa_afrika_watoa_wito_wa_kusitishwa_vita_nchini_drc
Rais wa Angola na wawakilishi kadhaa wa Umoja wa Afrika wametoa wito wa kusitishwa mapigano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya mkutano na Rais Felix Tshisekedi.
(last modified 2026-02-10T14:01:22+00:00 )
Feb 10, 2026 14:01 UTC
  • Umoja wa Afrika watoa wito wa kusitishwa vita nchini DRC
    Umoja wa Afrika watoa wito wa kusitishwa vita nchini DRC

Rais wa Angola na wawakilishi kadhaa wa Umoja wa Afrika wametoa wito wa kusitishwa mapigano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya mkutano na Rais Felix Tshisekedi.

Kwenye taarifa yake, mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na rais wa Angola, Joao Lorenco amesema amezitolea wito pande zinazovutana kwenye mzozo nchini humo kutangaza muda rasmi waliokubaliana wa kuanza usitishaji wa mapigano.

Tshisekedi alisaini taarifa hiyo sambamba na Rais wa Togo Faure Gnassingbe na Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo walioteuliwa kama wapatanishi wa Umoja wa Afrika na wawezeshaji wa mchakato wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Viongozi hao pia waliunga mkono makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Marekani na kusema Angola italazimika "kuanzisha mashauriano na pande zote zinazohusika na Kongo".

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo jana alifanya ziara katika mji mkuu wa Angola, Luanda ambapo alijadili mgogoro unaoigawanya mashariki mwa DRC na wenzake wa Angola na Togo.

Kwa Félix Tshisekedi, sehemu ya ziara yake ya Luanda ilikuwa kituo cha mwisho katika ziara ndefu ya kidiplomasia ambayo tayari imempeleka Togo, Kongo-Brazzaville, Uswisi, Ufaransa, Falme za Kiarabu, na Marekani tangu mwanzoni mwa mwaka 2026.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikimtuhumu jirani yake Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yanakanushwa na Kigali, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo linaendelea kuwa miongoni mwa maeneo yenye hali tete zaidi kiusalama, huku zaidi ya raia 60 wakiripotiwa kuuawa tangu mwanzoni mwa mwaka huu (2026) katika maeneo ya Beni na Lubero, kwa mujibu wa mashirika ya kiraia.