Kwa nini China inatetea "haki ya nyuklia" ya Iran?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i136410-kwa_nini_china_inatetea_haki_ya_nyuklia_ya_iran
China kwa mara nyingine tena imesisitiza juu ya kutetea haki ya nyuklia ya Iran.
(last modified 2026-02-09T02:23:59+00:00 )
Feb 09, 2026 02:23 UTC
  • Kwa nini China inatetea

China kwa mara nyingine tena imesisitiza juu ya kutetea haki ya nyuklia ya Iran.

Liu Bin, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China katika mazungumzo yake na Kazem Gharibabadi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia Masuala ya Sheria na Mahusiano ya Kimataifa na ambaye pia alisafiri nchini China kama mwakilishi maalum wa Rais wa Iran, siku ya Alhamisi, Februari 5, kwa mara nyingine tena ameunga mkono haki ya Tehran ya kutumia kwa amani nishati ya nyuklia na kusisitiza haja ya kupatiwa suala hilo ufumbuzi wa kisiasa na kidiplomasia.

Kwa mujibu wa tovuti ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China, afisa huyo wa China alisema kuwa, Beijing daima imekuwa ikiunga mkono utatuzi wa amani wa suala la nyuklia la Iran. Alisema Beijing inapinga tishio la kutumia nguvu na kuweka vikwazo, na kuongeza: 'China inaunga mkono haki halali ya Iran ya kutumia nishati ya nyuklia kwa njia ya amani.' Liu Bin amekumbusha kuwa Iran imesisitiza mara kwa mara msimamo wake wa kutotengeneza silaha za nyuklia na kwamba China iko tayari kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kuendelea kuhimiza ufumbuzi unaofaa na wa kiadilifu kwa suala hilo.

Katika mazungumzo hayo, Gharibabadi pia amepongeza msimamo wa China wa kutoegemea upande wowote na wa haki kuhusu suala la nyuklia la Iran, na kusisitiza hamu ya Tehran ya kudumisha mawasiliano na uratibu endelevu na Beijing.

Uteteaji wa wazi wa China wa "haki ya nyuklia ya Iran" hasa katika mwaka huu wa 2026, na kwa kuzingatia kuongezeka mivutano ya Marekani na Iran kuhusu suala la nyuklia, unapaswa kutathminiwa na kueleweka katika mfumo mpana zaidi wa sera za nje za Beijing. Mfumo huo unachanganya masuala ya kisheria, kijiopolitiki, kiuchumi na ushindani wa kimuundo na nchi za Magharibi. Kwa kawaida China hujaribu kuwasilisha misimamo yake si kama uungaji mkono wa kisiasa kwa taifa fulani, bali kama uteteaji wa kanuni kuu za mfumo wa kimataifa, kama vile haki ya matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia, ushirikiano wa pande nyingi na kupinga mashinikizo ya upande mmoja.

Liu Bin (kulia) akiwa na Kazem Gharibabadi

Moja ya sababu kuu na muhimu kwa China ni kusisitiza utawala wa sheria za kutoeneza silaha za nyuklia. Kwa mtazamo wa Beijing, Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia NPT ni "kifurushi cha haki na wajibu". Hii ina maana kwamba nchi zinazojitolea kutotengeneza silaha za nyuklia, zina haki pia ya kunufaika na teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani. Kwa kutilia maanani suala hilo, China inahoji kuwa kuiwekea vikwazo Iran zaidi ya ahadi zake zinazokubalika ni ukiukaji wa mwelekeo na matakwa ya mkataba huo. Kutetea haki ya nyuklia ya Iran katika muktadha huu, kwa China, ni kutetea mfumo wa sheria za kimataifa, ambapo yenyewe pia inanufaika nao.

Sababu nyingine ni ushindani wa kijiopolitiki wa China na Marekani na washirika wake wengine wa Magharibi. Katika miaka ya hivi karibuni, Beijing imezidi kupinga kile inachokiita "sera za vikwazo, mashinikizo na uingiliaji wa upande mmoja". Kwa China, kadhia ya nyuklia ya Iran ni mfano wa wazi wa matumizi mabaya ya vikwazo na mifumo ya kisiasa ili kufikia matakwa ya madola ya Magharibi. Kwa hivyo, hatua ya China kutetea Iran inachukuliwa pia kuwa ni ujumbe unaoelekezwa kwa mfumo wa kimataifa unaoongozwa na Marekani kwamba Beijing haiungi mkono siasa za upande mmoja katika utatuzi wa migogoro ya dunia.

Jambo la tatu ni maslahi ya kiuchumi na nishati. Iran ni miongoni mwa wadau muhimu katika soko la nishati na pia katika mpango wa "Ukanda Mmoja na Njia Moja". Uthabiti wa Iran na utatuzi wa kidiplomasia wa suala la nyuklia unatoa uwezekano wa ushirikiano wa muda mrefu wa kiuchumi kwa China. Kwa mtazamo wa Beijing, mashinikizo ya nyuklia na kiusalama sio tu kwamba yanadhoofisha uthabiti wa eneo, bali pia yanasababisha kuyumba kwa njia za nishati na biashara; Suala ambalo linakinzana moja kwa moja na maslahi ya kimkakati ya China.

Mwishowe, tunapasa kusema kwamba kwa kutetea haki ya nyuklia ya Iran, China inajaribu kuimarisha nafasi yake kama nguvu kubwa inayowajibika na wakati huohuo mpatanishi mwadilifu. Kwa kawaida Beijing hupendelea masuluhisho ya kidiplomasia, mazungumzo na kurejea kwenye mikataba ya kimataifa, jambo linalofanya mbinu hii kuwavutia wengi mkabala wa siasa za mabavu na za upande mmoja za nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani. Kwa maana hiyo, msimamo wa China sio tu kwamba ni wa kuitetea Iran moja kwa moja, bali ni sehemu ya juhudi pana zaidi za kufafanua upya nafasi yake katika mfumo wa dunia, ambapo inataka kuwa mtetezi wa sheria za kimataifa na wakati huo huo kuwa mkosoaji wa upendeleo na ubaguzi unaofanywa na nchi za Magharibi kuhusu suala hilo.