Jun 14, 2024 14:39 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Amali za Hija zinawatia wahaka maadui

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema amali za ibada tukufu ya Hija zinawatia hofu na wasiwasi mkubwa maadui.

Tovuti ya Kiongozi Muadhamu (Khamenei.ir) imechapisha sehemu ya ujumbe wa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei utakaotolewa kesho Jumamosi kwa Mahujaji, kwa mnasaba wa Hija ya mwaka huu.

Sehemu ya ujumbe huo wa Kiongozi Muadhamu inasema: Unapotafakari kuhusu mkusanyiko huu adhimu wa kustaajabisha, na amali za ibada ya Hija, ni chimbuko la kuongezeka imani na yakini kwa Waislamu, na wakati huohuo, ni tishio na sababu ya kuingiwa na hofu maadui.

Kipande kimoja cha ujumbe huo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Mahujaji kimeashiria kadhia ya 'Kujibari na Washirikina' ambayo ni sehemu muhimu ya ibada ya Hija ya kila mwaka.

Mahujaji katika Nyumba Tukufu ya Allah mjini Makka

Ayatullah Ali Khamenei amesema: Kujibari na Mushirikina mwaka huu kunapasa kuvuka mipaka ya wakati na zama kwa Waislamu kutoka miji na nchi mbalimbali kote duniani.

Ujumbe huo umeendelea kusema: Kujiweka mbali na washirikina kunaihusu jamii yote ya mwandamu na wala si Mahujaji tu.

Zaidi ya Waislamu milioni 2 wamewasili Saudi Arabia kutekeleza ibada ya Hija mjini Makka mwaka huu. Hija ambayo ni moja ya mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini ulimwenguni mwaka huu imerejea katika uwezo wake kamili kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa janga la corona miaka mitatu iliyopita.

Waislamu wote wenye uwezo wa kimwili na kimali wanatakiwa kuhiji angalau mara moja katika maisha yao.

 

 

 

Tags