Nchi nyingine ya Afrika yataka kujiunga na jumuiya ya BRICS
(last modified Thu, 20 Jun 2024 02:51:10 GMT )
Jun 20, 2024 02:51 UTC
  • Nchi nyingine ya Afrika yataka kujiunga na jumuiya ya BRICS

Zimbabwe imesema iko tayari kujiunga na jumuiya ya kiuchumi ya BRICS, ambayo itatoa fursa nzuri kwa nchi hiyo kufanya biashara katika mazingira huru na nchi nyingine wanachama.

Oppah Muchinguri-Kashiri, Waziri wa Ulinzi wa Zimbabwe amenukuliwa na gazeti la The Herald linalomilikiwa na serikali ya Harare akisema kuwa, nchi hiyo ipo katika mchakato wa kuomba uanachama katika jumuiya ya BRICS.

Amesema Zimbabwe kama mataifa mengine yaliyotangaza azma zao, inatambua nafasi ya jumuiya ya BRICS katika kubadili mlingano wa nchi za Magharibi. Waziri wa Ulinzi wa Zimbabwe ameongeza kuwa, taifa hilo la kusini mwa Afrika liko tayari kujiunga na muungano wowote ambao una malengo ya ujengaji na yaliyoainishwa vyema.

Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe kutangaza azma ya nchi yake kujiunga na BRICS, katika mahojiano na shirika la TASS pambizoni mwa mkutano wa kiuchumi wa St. Petersburg International Economic Forum (SPIEF).

Kundi la BRICS la nchi zinazoinukia kiuchumi, ambalo hadi hivi karibuni lilikuwa na wanachama wake wakuu watano tu, ambao ni Brazil, Russia, India, China, na Afrika Kusini, lilipata upanuzi mkubwa Januari mwaka huu wakati Iran, Ethiopia, Misri na Muungano wa Falme za Kiarabu zilipojiunga nalo.

Saudi Arabia pia imealikwa na iko tayari kuwa mwanachama. Mataifa mengine mengi yameonyesha nia ya kujiunga huku mengine yakiwa tayari yameshatuma maombi rasmi.

Kulingana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), BRICS kwa sasa inachangia kiasi cha 36% ya Pato la Taifa la Kimataifa katika suala la usawa wa uwezo wa kununua (PPP), ikilinganishwa na takribani 30% ya kundi la G7 la nchi zilizoendelea kiuchumi.

Tags