Jun 21, 2024 07:49 UTC
  • Iran yamuita balozi wa Italia kulalamikia hatua ya Canada dhidi ya IRGC

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imemuita balozi wa Italia mjini Tehran ambaye anawakilisha pia maslahi ya Canada hapa nchini, kulalamikia hatua ya serikali ya Ottawa ya kuliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kwenye orodha ya kile inachokiita "makundi ya kigaidi".

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema, balozi huyo wa Italia aliitwa katika wizara hiyo jana Alkhamisi na kukabidhiwa malalamiko rasmi ya Iran dhidi ya hatua ya kisiasa na isiyo ya busara ya serikali ya Canada ya kulitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni la kigaidi. 

Aidha balozi huyo wa Italia mjini Tehran ambaye anawakilisha pia maslahi ya Canada hapa nchini, ametakiwa kuitaarifu Ottawa kuwa Tehran itachukua hatua za kujibu mapigo ya kitendo hicho kisicho cha kidiplomasia cha Ottawa.

Kabla ya hapo, Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran sambamba na kulaani vikali hatua hiyo ya uadui ya serikali ya Canada dhidi ya Jeshi la IRGC, alieleza kwamba, kitendo hicho ni katika mfululizo wa hatua za Ottawa za kuuunga mkono utawala wa kigaidi wa Israel.

Askari wa jeshi la SEPAH

Katika ujumbe alioutuma jana Alkhamisi kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa X, Kani alieleza bayana kuwa, jeshi la IRGC limekabiliana na magaidi na kuzima shari za magaidi katika eneo la Asia Magharibi.

Alisisitiza kuwa, hatua hiyo ya Canada ni zawadi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, magaidi na maadui wengine wa amani na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi.

 

Tags