Jun 21, 2024 12:37 UTC
  • Michael Usi ateuliwa kuwa Makamu mpya wa Rais Malawi baada ya kifo cha Saulos Chilima

Rais Lazarus Chakwera wa Malawi amemteua Michael Usi kuwa makamu mpya wa rais wa nchi hiyo kuchukua nafasi ya Saulos Chilima aliyefariki katika ajali ya ndege tarehe 10 mwezi huu wa Juni.

Rais Chakwera ametangaza habari hiyo kupitia Katibu wa Rais na wa  Baraza la Mawaziri, Colleen Zamba, na ilikuwa imepangwa kwamba makamu huyo mpya wa rais ataapishwa leo Ijumaa.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais, Usi alikuwa waziri wa maliasili na mabadiliko ya tabia nchi wa Malawi. Pia ni makamu mwenyekiti wa chama cha United Transformation Movement ambacho Chilima alikianzisha na kukiongoza akiwa rais.

Usi aliyezaliwa mwaka 1968, anajulikana kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya burudani kama mwigizaji, mwandishi wa tamthilia na mtengenezaji wa filamu. Anajulikana pia kwa kazi zake za maendeleo nchini Malawi.

Mbali na kazi yake ya burudani, Usi ana uzoefu mkubwa na mashirika yasiyo ya kiserikali hasa katika kuendesha miradi ya jamii kwenye sekta za afya, elimu na maendeleo ya kiuchumi.

Katika maisha yake yote, Usi amekuwa mtetezi wa haki za kijamii, elimu na uwezeshaji wa jamii, na hivyo kumpa heshima na umaarufu mkubwa miongoni mwa wananchi wa Malawi.

Uteuzi wake unaripotiwa kuonekana kama hatua ya kimkakati ya kutumia haiba na uzoefu wake ili kutatua changamoto za Malawi na kukuza mipango ya maendeleo.