Jun 27, 2024 12:42 UTC
  • Kanani: Iran ni mbeba bendera ya mapambano ya dunia dhidi ya magenge hatari ya mihadarati

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza juu ya irada madhubuti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kupambana na tishio la dunia la madawa ya kulevya.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeitaja tarehe 26 Juni kuwa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Madawa ya Kulevya. Siku hii imepewa jina hili lengo likiwa ni kubainisha azma ya kisiasa ya nchi mbalimbali katika vita dhidi ya madawa ya kulevya katika jamii, kuyadhibiti na kuchukua hatua za kimataifa kuhusu mapambano dhidi ya biashara ya mihadarati. 

Kuhusiana na suala hili, Nasser Kanani Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameandika katika ukurasa wake wa X kwamba: Katika Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Mihadarati Duniani; Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa mbeba bendera ya mapambano ya kimataifa dhidi ya wauza madawa ya kulevya kwa mara nyingine inasisitiza azma yake ya kukabiliana na tishio hilo la kimataifa. 

Iran, mbeba bendera ya vita dhidi ya madawa ya kulevya 

Msemaji wa chombo cha diplomasia cha Iran ameongeza kuwa: Ushirikiano wa karibu wa Iran na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), kufa shahidi maelfu ya raia wa nchi,  kugharamika pakubwa kimaada na kimaanawi na kukamata kiwango kikubwa cha dawa za kulevya katika eneo hili hatarishi la kijiografia yote haya yanaashiria irada thabiti ya Iran ya kukabiliana na tishio hilo la dunia.