Jun 27, 2024 02:29 UTC
  • Kutoweka watoto katika Ukanda wa  Gaza

Kwa mujibu wa ripoti mpya zilizochapishwa na shirika la kimataifa linaloitwa "Save the Children", watoto wapatao elfu 21 wa Kipalestina wametoweka huko Ukanda wa Gaza, ambapo watoto elfu 17 wametenganishwa na familia zao kutokana na vurugu zilizosababishwa na vita, hasa operesheni za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni katika ukanda huo.

Watoto wengine elfu nne pia wamenaswa chini ya vifusi na idadi isiyojulikana wamekamatwa na vikosi vya utawala wa Kizayuni au kuzikwa katika makaburi yasiyojulikana.

Kwa kutilia maanani kwamba jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza zingali zinaendelea kwa kasi kamili, bila shaka takwimu kamili zinazohusiana na hali ya watoto katika ukanda huo ni kubwa zaidi kuliko zilizotangazwa rasmi. Hasa ikizingatiwa kuwa jinai za utawala wa Kizayuni huko  Gaza ni mfano wa wazi wa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wanaodhulumiwa na watoto ndio walengwa wakuu wa jinai hizo za Wazayuni katika Ukanda wa Gaza.

Muqawama wa wananchi wa Ukanda wa Gaza dhidi ya jinai za Wazayuni si tu kwamba umetoa pigo kubwa kwa Wazayuni, bali pia umemuweka Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu mhalifu wa utawala wa Kizayuni katika hali ngumu sana ya ndani, ambapo hana budi ila kuendeleza uhalifu na jinai zake hizo dhidi ya watu wasio na ulinzi.

Ali Daneshnia, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusu suala hilo:  "Bemjamini Netanyahu alianzisha jinai huko Gaza akiwa na malengo matatu makuu kwanza kabisa, kuiangamiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, pili kukombolewa mateka wa Kizayuni na tatu, kuondoka katika Ukanda wa Gaza na ushindi, lakini kivitendo, si tu kwamba hajafikia hata moja ya malengo hayo bali mwenyewe hivi sasa anaandamwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kama mtendajinai za kivita baada ya kuendesha wimbi la mauaji ya umati dhidi ya watu wa Gaza, suala ambalo limeibua kashfa kubwa dhidi yake katika majukwaa ya kimataifa. Jinai za Wazayuni huko Gaza zimeibua wasiwasi mkubwa zaidi ulimwenguni kutokana na ukweli kwamba mashirika ya Kimataifa yanaonya kuwa athari za kimwili na kisaikolojia za jinai za Wazayuni huko Gaza kwa watoto zitaendelea kushuhudia katika vizazi kadhaa vijavyo.

Save the Children, huduma za afya kwa watoto huko Gaza

Kwa kauli ya Elizabeth White, mkurugenzi wa uhusiano wa umma wa shirika la Save the Children, kutokuwepo huduma za afya kwa watoto wa Gaza ni janga kubwa mno.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza, watoto wanaendelea kufa kutokana na utapiamlo. Hospitali za ukanda huo zimeharibiwa na hazina uwezo wa kutoa huduma kwa waathirika wala mafuta ya kuendeshea shughuli zake za kawaida.

Wakati huo huo, Matthew Miller, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani katika kujibu ukosoaji wa Benjamin Netanyahu aliyedai kuwa Marekani inachelewesha kuutumia utawala huo ghasibu silaha, alisisitiza kuwa; 'Washington itaendelea kuipa Tel Aviv silaha bila kuchelewa.' Hii ina maana kwamba kwa kuendelea kuupa utawala huo wa Kizayuni uungaji mkono usio na masharti na wa pande zote, si tu kuwa Marekani inazuia usitishaji vita huko Gaza, bali pia inashiriki kikamilifu katika jinai na mauaji ya umati ya utawala huo dhidi ya watu wa Gaza.

Kwa kadiri kwamba kufikia sasa, utawala huo umeua shahidi takriban Wapalestina 37,000 katika Ukanda wa Gaza, hasa wanawake na watoto, jinai ambazo zingali zinaendelea kwa uungaji mkono na ushirikiano kamili wa Marekani.