Jun 20, 2024 02:50 UTC
  • Wasiwasi wa nchi za Magharibi kuhusu safari ya Rais Vladimir Putin nchini Korea Kaskazini

Katika mkesha wa safari yake nchini Korea Kaskazini, Rais Vladimir Putin wa Russia aliandika katika makala kwamba nchi mbili hizo zinaelekea kwenye ushirikiano wa karibu na umoja licha ya kuwepo mashinikizo ya nchi za Magharibi.

Vyombo vya habari vya Russia vimeripoti kuwa Rais Vladimir Putin ameandika katika makala katika gazeti la Rodong Sinmun la Korea Kaskazini kwamba ushirikiano wa karibu kati ya Moscow na Pyongyang utaimarisha mamlaka yao ya kujitawala na kuziunganisha nchi mbili katika kukabiliana na mashinikizo ya Magharibi.

Ni kwa sababu hiyo ndipo, katika mkesha wa safari ya Putin nchini Korea Kaskazini, Marekani na Jeshi la Nchi za Magharibi (NATO) zikaelezea wasiwasi wao kuhusu eti madhara ya kuimarishwa ushirikiano kati ya Moscow na Pyongyang. Safari hiyo inazitia wasiwasi mkubwa nchi za Magharibi kwa sababu, kwa mtazamo wa Rais wa Russia, Korea Kaskazini ni "mshirika imara aliye na fikra zinazofanana" na za Russia na itaendelea kuwa hivyo katika siku zijazo.

Safari ya kwanza ya Rais Putin (kulia) nchini Korea Kaskazini baada ya miaka 24

Mustafa Ghasemi, Mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema kuhusu suala hilo:

"Kwa kuzingatia baadhi ya tofauti zilizopo kati ya Russia, China na Korea Kaskazini kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisiasa na kijeshi, nchi za Magharibi hazikuwahi kufikiria kwamba kwa kutoa mashinikizo na kutekeleza vikwazo vya kijeshi dhidi ya nchi hizo tatu, zingeweza kuzifanya zishirikiane kwa karibu na kuwa na umoja kama ilivyo hivi sasa. Kwa hivyo kuimarika ushirikiano wa kijeshi na kiulinzi wa Moscow, Beijing na Pyongyang katika hali ambayo Russia inazikabili nchi za Magharibi katika vita vya Ukraine, ni jambo linalozitia wasiwasi mkubwa Marekani na (NATO)."

Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndipo, Putin akasema wazi kwamba anathamini na kushukuru sana uungaji mkono usioyumba wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea kwa kuunga mkono operesheni maalum za kijeshi za Russia huko Ukraine, mshikamano wake na Russia katika maswala muhimu ya kimataifa, na hamu yake ya kutetea vipaumbele na maono ya pamoja ya pande mbili katika Umoja wa Mataifa.

Wakati ulimwengu wote wa Magharibi umesimama upande wa Ukraine na kuiunga mkono dhidi ya Russia, ni wazi kuwa ushirikiano wa kijeshi na kiulinzi wa Korea Kaskazini, China na Russia unazitia wasiwasi mkubwa nchi za Magharibi. Kwa sababu hiyo, duru za kijeshi na kisiasa za Marekani na NATO zimeionya mara kwa mara China kuhusu misaada yake ya kijeshi kwa Russia katika vita na Ukraine.

Hivyo basi, ahadi ya Rais Vladimir Putin wa Russia, kwamba atapanua uhusiano wa Moscow na Pyongyang hadi kiwango cha juu kabisa na kuwa itaunga mkono juhudi za Korea Kaskazini za kujilinda dhidi ya "vitishio vya kijeshi, ulaghai na mashinikizo ya Marekani" inatia wasiwasi mkubwa kwa Marekani na washirika wake wa kieneo na kimataifa.

Nchi za Magharibi zina wasiwasi kuhusu safari ya Putin nchini Korea Kaskazini 

Hii ni kwa sababu Marekani inajaribu kutoa mashinikizo makali dhidi ya Korea Kaskazini kwa kuunda muungano wa nchi kadhaa dhidi ya Pyongyang ili kuilazimisha ijisalimishe kwa nchi za Magharibi. Haya yanajiri katika hali ambayo kwa mtazamo wa Putin, Moscow na Pyongyang zimekuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri katika miaka 70 iliyopita, ushirikiano ambao umejengeka katika msingi wa usawa, uaminifu na kuheshimiana pande mbili.

Kwa maelezo hayo, wakati wa kufanyika safari ya Putin nchini Korea Kaskazini wiki hii, hati kadhaa za maelewano ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili zimetiwa saini, mojawapo ikiwa ni "mkataba wa ushirikiano wa kistratijia".

Kwa vyo vyote vile, safari ya Putin nchini Korea Kaskazini inafanyika huku Moscow na Pyongyang zikiwa chini ya vikwazo vikali vya nchi za Magharibi na kuimarika uhusiano wao kumezusha wasiwasi mkubwa barani Ulaya na  Marekani.

Nchi za Magharibi zinadai kuwa Korea Kaskazini inaipa Russia silaha ambazo inazitumia katika vita dhidi ya Ukraine, madai ambayo yamepingwa vikali na serikali za Moscow na Pyongyang. Licha ya kuwa ulimwengu wa Magharibi umesimama kwa kauli moja na Ukraine na kuipa Kyiv kila aina ya silaha ili kukabiliana na Russia, lakini sasa unadhihirisha wasiwasi wake hadharani kuhusu kuimarika ushirikiano wa Moscow na Pyongyang, kwa sababu misaada hiyo ya kijeshi kwa Ukraine imeshindwa kubadilisha hali ya mambo katika medani ya vita kwa manufaa ya Kyiv.