Jun 20, 2024 12:29 UTC
  • Iran yalaani hatua ya Canada ya kuliweka jeshi la SEPAH katika orodha ya magaidi

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amelaani vikali hatua ya uadui ya serikali ya Canada dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH).

Nasser Kanani Chafi, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran, amelaani vikali hatua ya kisiasa, isiyo ya kawaida na isiyo ya busara ya serikali ya Canada ya kulitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni la kigaidi.

Kan'ani amesema, uamuzi huo wa Canada usio wa busara ni hatua ya chuki na kinyume na viwango na kanuni zinazokubalika za sheria za kimataifa za kutoingilia masuala ya ndani ya serikali na mfano wa wazi wa hujuma dhidi ya mamlaka ya kitaifa ya Iran.

 

Kan'ani Chafi amesema, hatua ya kutowajibika na ya kichochezi ya serikali ya Canada iko kwenye mkondo ghalati na usio sahihi ambao imeuchukua kwa zaidi ya muongo mmoja chini ya ushawishi wa makundi mbalimbali ya watu wanaochochea vita na wavunjaji halisi wa haki za binadamu na waasisi wakuu wa ugaidi.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameeleza kwamba, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) ni taasisi ya kiutawala iliyotokana na muktadha wa taifa la Iran na ina utambulisho rasmi na wa kisheria unaotokana na katiba ya Jamhuri ya Kiislamu, ambayo, pamoja na vipengele vingine vya jeshi, ina jukumu la kulinda usalama wa taifa na mipaka ya Iran, pamoja na kuchangia kwa usalama imara na utulivu katika eneo ili kukabiliana na ugaidi.

Tags