Kadhaa wauawa na kujeruhiwa Nigeria katika shambulio la Boko Haram
Kwa akali watu tisa wameuawa huku wengine wanne wakijeruhiwa katika shambulizi la magaidi wa Boko Haram dhidi ya jamii ya Malam Fatori katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Sugun Mai Mele, kamishna wa serikali za mitaa katika eneo hilo, amesema shambulio hilo lilitokea yapata kilomita 270 (maili 167) kutoka Maiduguri, mji mkuu wa jimbo hilo.
Afisa huyo ameongoza ujumbe kwa niaba ya Gavana wa jimbo la Borno, Babagana Umara Zulum, ambaye kwa sasa yuko katika safari rasmi nje ya nchi, kuomboleza na familia za wahaanga wa hujuma hiyo.
"Tuko hapa kwa niaba ya Mheshimiwa, Gavana Babagana Umara Zulum, ambaye yuko nje ya nchi kwa shughuli rasmi, kuwapa pole watu wa jamii ya Malam Fatori kwa shambulio la kusikitisha la hivi majuzi," imesema taarifa. Amesisitiza kuwa, serikali ya jimbo la Borno na wanajeshi watafanya kila linalowezekana ili kuilinda jamii hiyo.
"Malam Fatori ni eneo moja la serikali za mitaa ambalo tumejitolea kuhakikisha linakuwa na utulivu kwa sababu ya umuhimu wake wa kimkakati, na kuwataka wananchi kuwa wastahimilivu zaidi na wafanye maombi ili kuepusha matukio kama haya katika siku zijazo," imesema taarifa hiyo.
Haya yanajiri wiki chache baada ya magaidi 20 kuuawa katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na jeshi la Nigeria katika jimbo la kaskazini la Zamfara.