Russia: Wamagharibi karibuni watamtosa Rais Zelensky wa Ukraine
(last modified Fri, 21 Jun 2024 02:15:09 GMT )
Jun 21, 2024 02:15 UTC
  • Russia: Wamagharibi karibuni watamtosa Rais Zelensky wa Ukraine

Idara ya Intelijensia ya Nje ya Russia (SVR) imefichua kuwa, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine ni mwanasiasa tegemezi kwa Magharibi, na kwamba karibuni hivi, Marekani pamoja na waitifaki wake 'watamtoa kafara' kiongozi huyo pasi na kujali kitu chochote.

Taarifa iliyotolewa jana Alkhamisi na idara hiyo ya intelijensia ya Russia imeeleza kuwa, "Ikulu ya White House ya Marekani karibuni itafunga mradi wa Zelensky."

Imeeleza kuwa: Ikulu ya White House ikishamtumia Zelensky, itamtupa jaani kama taka bila kufikiria mara mbili, kisha nafasi yake ichukuliwe na mwanasiasa mwingine wa Ukraine ambaye (Washington) inamuona kuwa ataweza kuongoza mazungumzo ya kupatiwa ufumbuzi mgogoro na Russia kwa njia ya amani.

Idara ya Intelijensia ya Nje ya Russia imedokeza kuwa, yumkini Wamagharibi wakiongozwa na Marekani wakamtosa Zelensky na badala yake wamsimike madarakani Jenerali mstaafu Valery Zaluzhny, aliyekuwa kamanda mwandamizi wa jeshi la Ukraine.

Rais Joe Biden wa Marekani (kushoto) akihutubu

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine ambaye amekuwa akiwashinikiza viongozi wa Magharibi waipe Kiev silaha na vifaa zaidi vya kijeshi kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya Moscow, yupo madarakani kinyume cha sheria, kwani muhula wake wa miaka mitano ulimalizika Mei mwaka huu.

Haya yanajiri siku chache baada ya Katibu Mkuu wa shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO, Jens Stoltenberg kusema kuwa muugano huo hauna mpango wa kutuma wanajeshi wake nchini Ukraine, na kwamba jumuiya hiyo ya kijeshi ya Magharibi haiitazami Russia kama tishio la kijeshi kwa nchi za Magharibi. 

Tags