Jun 20, 2024 07:10 UTC
  • Ushindi mwingine mkubwa kwa HAMAS, jeshi la Israel latangaza rasmi haliwezi kuifuta, Netanyahu aja juu

Msemaji wa Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel (IDF), Daniel Hagari alisema jana Jumatano kwamba Hamas haiwezi kufutwa na amependekeza kufikiwe makubaliano ya kubadilishana mateka kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha mateka wote wa Israel wanaoshikiliwa huko Ghaza wanaachiliwa huru.

Matamshi hayo ya kukiri rasmi jeshi la Israel kuwa haliwezi kuimaliza HAMAS bali harakati hiyo imeundwa ili ibakie huko Ghaza, ni ushindi mwingine mkubwa kwa harakati hiyo ya Kiislamu ambayo kwa zaidi ya miezi minane sasa inapambana kiume mbele ya mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni.

Msemaji wa jeshi la Israel amekiri kuwa hawaiwezi HAMAS katika mahojiano aliyofanyiwa na kanali ya 13 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni na hii ni mara ya kwanza kwa afisa wa Israel kusema kuwa harakati hiyo ya Kiislamu ya Wapalestina haishindiki.

Matamshi hayo yamemhamakisha waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu ambaye moja ya malengo ya kuanzisha vita vya kikatili huko Ghaza ni eti kuimaliza nguvu HAMAS.

Msemaji wa jeshi la Israel amesema, "Hamas ni fikra, Hamas ni taasisi. Hamas imekita mizizi katika mioyo ya watu -- yeyote anayefikiri tunaweza kuiondoa Hamas anakosea." 

Wanajeshi makatili wa Israel wamekuwa wakifanya mauaji ya kutisha kwenye Ukanda wa Ghaza kwa zaidi ya miezi minane sasa, na kusababisha janga kubwa la kibinadamu mbali na uharibifu mkubwa na kuua zaidi ya watu 37,300 hasa raia wa kawaida, wengi wao wakiwa ni watoto wadogo.