Waandamanaji wakusanyika Marekani baada ya afisa wa uhamiaji kutekeleza mauaji
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135936-waandamanaji_wakusanyika_marekani_baada_ya_afisa_wa_uhamiaji_kutekeleza_mauaji
Umati wa watu umekusanyika Minneapolis, Marekani kupinga uwepo wa maafisa wa uhamiaji wa shirikisho katika jimbo hilo, baada ya kupigwa risasi na kuuawa Alex Pretti mwenye umri wa miaka 37.
(last modified 2026-01-26T23:03:11+00:00 )
Jan 26, 2026 23:03 UTC
  • Waandamanaji wakusanyika Marekani baada ya afisa wa uhamiaji kutekeleza mauaji

Umati wa watu umekusanyika Minneapolis, Marekani kupinga uwepo wa maafisa wa uhamiaji wa shirikisho katika jimbo hilo, baada ya kupigwa risasi na kuuawa Alex Pretti mwenye umri wa miaka 37.

Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu wamelaani mauuaji hayo na kutaka sharia ifuate mkondo wake na kuhakikisha wahusika wa mauaji hayo wanachukuliwa hatua.

Maandamano hayo yamesambaa kwa kasi hadi katika miji ya Portland, Maine, San Francisco na Washington DC. Serikali iko chini ya shinikizo kubwa la ndani, huku wananchi wakidai haki, uwazi na kuheshimiwa kwa utu wa raia.

Gavana wa Minnesota Tim Walz ametoa wito kwa Rais wa Marekani, Donald Trump kuwaondoa maafisa hao wa shirikisho katika jimbo lake, akisema: "Huu ni wakati wa mabadiliko."

Marais wa zamani wa Marekani Barack Obama na Bill Clinton, wametoa wito kwa Wamarekani kusimama na kutetea maadili ya nchi yao baada ya mauaji ya pili ya raia mjini Minneapolis.

Serikali ya Trump imekuwa ikikabiliwa na shinikizo linaloongezeka kuhusu msako wake mkali dhidi ya wahamiaji, hasa baada ya maafisa wa shirikisho kumpiga risasi na kumuua Alex Pretti, muuguzi wa chumba cha wagonjwa mahututi mwenye umri wa miaka 37, siku ya Jumamosi, wakati wakijibizana naye kwenye barabara yenye barafu.

Tukio hilo lilitokea chini ya wiki tatu baada ya afisa wa uhamiaji kumpiga risasi na kumuua Renee Good, naye akiwa na miaka 37, ndani ya gari lake katika mji huo huo wa Kati-Magharibi.

Video iliyosambaa sana kwenye mitandao ya kijamii na kuthibitishwa na vyombo vya habari vya Marekani ilionyesha kuwa Pretti hakutoa silaha yoyote, na maafisa walimpiga risasi sekunde chache baada ya kummwagia usoni kemikali inayowasha na kumtupa chini.