Russia yaionya Marekani kuhusu chokochoko yoyote dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135942-russia_yaionya_marekani_kuhusu_chokochoko_yoyote_dhidi_ya_iran
Serikali ya Russia imeionya Marekani kuhusiana na kuanzisha chokochoko yoyote ya kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2026-01-26T23:05:24+00:00 )
Jan 26, 2026 23:05 UTC
  • Russia yaionya Marekani kuhusu chokochoko yoyote dhidi ya Iran

Serikali ya Russia imeionya Marekani kuhusiana na kuanzisha chokochoko yoyote ya kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Msemaji wa ikulu ya Rais wa Russia (Kremlin) ameonya juu ya matokeo mabaya ya kikanda na kimataifa ya chokochoko yoyote ile dhidi ya Iran.

Dmitry Peskov msemaji wa ikulu ya Russia Kremlin ametoa onyo hilo katika mkutano wake na waandishi wa habari na kubainisha kwamba, "Shambulio lolote tarajiwa dhidi ya Iran litasababisha ukosefu wa utulivu katika eneo la Asia Magharibi."

Huku Rais Donald Trump wa Marekani akiendelea na bwabwaja zake dhidi ya Iran, weledi wa mambo wanauchukulia uropokaji huo kuwa ni sehemu ya vita vya kisaikolojia vya Washington vya kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu kusalimu amri mbele ya ubabe na siasa za kupenda makuu za Ikulu ya Marekani.

Katika kujibu uropokaji huo wa Trump dhidi ya Iran, makundi mbalimbali ya muqawama yametangaza kuwa, chokochoko yoyote ya kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu itapelekea kuripuka moto mkubwa na kulikumba eneo zima la Asia Magharibi.

Wajumbe wa Bunge la Congress la Marekani huku wakipinga chokochoko yoyote ya utawala wa Trump katika eneo la Asia Magharibi, wameonya juu ya athari za vitendo hivi kuwa na taathira hasi kwa bei ya nishati na usalama wa askari wa Marekani.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikisisitiza kwamba inataka amani na nchi zote duniani, lakini itajibu kwa nguvu zake zote chokochoko ndogo kabisa dhidi ya ardhi yake.