Jun 21, 2024 02:14 UTC
  • Umoja wa Mataifa watoa onyo kali kuhusu kuongezeka majanga katika Ukanda wa Gaza

Francesca Albanese, Ripota wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina, amesema katika taarifa kwamba hali ya maafa huko Ukanda wa Gaza imezidi kuwa mbaya. Kwa kauli yake, utawala haramu wa Israel unalenga misafara ya misaada ya kibinadamu inayotumwa Gaza na kuzuia ufikaji wa misaada katika ukanda huo.

Huku akieleza kuwa utawala wa Kizayuni unataka kuufuta kabisa Ukanda wa Gaza na kuufanya usiweze kukaliwa na watu, Albanese amesema tangu kuasisiwa kwake utawala katili wa Israel umekuwa ukiendesha kampeni ya kulipiza kisasi kwa ajili ya kuwaangamiza kabisa Wapalestina. Ripota huyo wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa pia amesisitiza kuwa jamii ya Palestina imekuwa ikisalitiwa na jumuiya ya kimataifa tangu 1948. Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Kibinadamu, hivi karibuni pia alitangaza kuwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza baada ya Oktoba 7, 2023 yamegeuza ukanda huo uliozingirwa wenye watu wahitaji kuwa Jahannam kwenye uso wa dunia.

Mashambulizi ya kinyama ya Wazayuni katika Ukanda wa Gaza

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu kushadidi hali mbaya ya Gaza kutokana na sisitizo la utawala wa Kizayuni la kuendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina kwa upande mmoja, na kuzuia misaada kuwafikia wakaazi madhulumu wa ukanda huo kwa ajili ya kuwaweka njaa na kuwaua taratibu kwa upande wa pili. Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, ambaye hivi karibuni alivunja baraza la mawaziri la vita, hivi sasa amechukua udhibiti kamili wa mchakato wa maamuzi kuhusu vita vya Gaza, ambapo amekataa kukubali mipango yoyote ya usitishaji vita ukiwemo ule uliowasilishwa na muitifaki wake mkuu wa kistartijia yaani Marekani na kupitishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, yaani azimio nambari 2735. Anaendeleza operesheni za kijeshi za mauaji ya umati huko Gaza, hasa katika mji wa  Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza, kwa kisingizio cha kuangamiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas na makundi mengine ya muqawama wa Palestina na eti kuachiliwa mateka wa Kizayuni.

Hata hivyo mashambulizi ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni hayajaleta lolote isipokuwa mauaji, uharibifu, kila aina ya jinai za kivita, kukiukwa sheria za kimataifa, kushambuliwa mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu na kusababisha njaa katika ukanda huo. Wakati huo huo, baada ya kupita zaidi ya miezi minane tangu utawala wa Kizayuni uvamie Ukanda wa Gaza bila ya matokeo wala mafanikio yoyote, utawala huo umezidi kunasa katika migogoro ya ndani na nje na hivyo kuzidi kutengwa kieneo na kimataifa.

Nukta muhimu ni kwamba hata Marekani ambayo ndiyo msambazaji mkuu wa kila aina ya silaha na mabomu yanayotumiwa na Israel kutekelezea mauaji ya halaiki dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Ukanda wa Gaza na kuharibiwa miundombinu ya ukanda huo, imelazimika kukiri kuhusu maafa na jinai za kivita zinazofanywa na utawala huo huko Gaza.

Katika muktadha huo, Samantha Power, mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani amesema: "Hali ya kibinadamu huko Gaza ni ngumu na ya kutisha sana ambapo hata Rais Joe Biden wa Marekani ameielezea kuwa ni Jahannam."

Katika salamu zake za Eid al-Adha kwa Waislamu, Biden bila ya kutaja ukatili wa utawala wa Kizayuni na silaha za Marekani zinazotumiwa na utawala huo ghasibu kwa ajili ya kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina, amekiri kwamba hadi sasa raia wengi wa kawaida, wakiwemo maelfu ya watoto, wamepoteza maisha huko Gaza. Familia zimekimbia makazi yao na sasa tunashuhudia jamii ya Wapalestina ikiteseka, kupitia machungu makali na kusambaratika.

Swali linalojitokeza hapa kuhusiana na ujumbe wa rais wa Marekani kwa mnasaba wa Eid al-Adh'ha ni kuwa je, ni kwa nini licha ya kukiri kuwa Wapalestina wanauawa kwa umati na utawala katili wa Israel, hachukui hatua zozote za kuzuia kuendelea mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Gaza, na je, kwa nini anaendelea kuutumia silaha utawala huo katili ili uendelee kuwachinja Wapalestina wasio na hatia?

Onyo jipya la UNICEF kuhusu janga la mauaji ya watoto huko Ukanda wa Gaza

Inaonekana kwamba ujumbe huo wa Biden kwa Waislamu umetolewa kwa ajili ya kupata uungaji mkono na kura za vijana, Waarabu na Waislamu wa Marekani katika uchaguzi mkuu ujao uliopangwa kufanyika mwezi Novemba na sio kuonyesha huruma kwa watu wa Ukanda wa Gaza.

Kwa hakika, ujumbe wa Joe Biden kwa mnasaba wa Eid al-Adha na kuashiria vita vya Ukanda Gaza ni sehemu ya kampeni yake ya uchaguzi ili apate kushinda uchaguzi wa mwaka huu. Biden anahitajia sana kura za Waislamu, hasa huko Michigan ili ashinde uchaguzi huo.

Tags