Jun 20, 2024 07:09 UTC
  • Iran yajibu shutuma zisizo na msingi za Marekani kuhusu Yemen

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amezitaja tuhuma za Marekani dhidi ya Iran kuhusu Yemen kuwa hazina msingi wowote na kusema kwamba, Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa ikitilia mkazo utatuzi wa amani wa mgogoro wa Yemen kupitia njia za kidiplomasia.

Kwa mujibu wa IRNA,  Amir Saeid Iravani, amesema hayo katika barua kwa mwenyekiti wa muda wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, madai yaliyotolewa na mwakilishi wa Marekani dhidi ya Iran katika mkutano wa wazi wa baraza hilo, hayana msingi wowote. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha kikao Juni 13, 2024 kuhusu hali ya Yemen.

Katika barua yake hiyo, Balozi Irafani amesema, kwa bahati mbaya, mwakilishi wa Marekani ametumia vibaya jukwaa la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama kawaida ya Washington, kutoa tuhuma dhidi ya nchi huru bila ya ushahidi wowote.

Ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakanusha vikali tuhuma zisizo na msingi za Marekani dhidi yake na kwamba mara kadhaa Tehran imetangaza kwamba inaheshimu kikamilifu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Yemen na haiingilii masuala ya ndani ya nchi hiyo bali dhamira yake yake kuu ni kuhakikisha mgogoro wa Yemen unatatuliwa kidiplomasia na kwa njia za amani.

Tags