May 10, 2024 07:59 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Kushiriki uchaguzi ni wajibu wa kitaifa wa kila mmoja

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kushiriki katika uchaguzi ni wajibu wa kitaifa kwa wananchi wote.

Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo mapema leo Ijumaa, mara baada ya kupiga kura yake katika duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge la 12 na kuongeza kuwa, "Hakuna tofauti kati ya uchaguzi mkuu na duru ya pili ya uchaguzi, yote yana umuhimu."

Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa, uchaguzi ni jambo muhimu kwa nchi na wananchi, na ni ishara ya ushiriki wa wananchi, fursa ya kufanya maamuzi yao, na kudhihirisha irada yao kwa taifa lao.

"Kadri kura zinavyokuwa nyingi, ndivyo Bunge linavyokuwa madhubuti na lenye nguvu, na kadri Bunge linavyokuwa na nguvu, ndivyo utendaji kazi ndani ya nchi unavyokuwa sahali," ameongeza Kiongozi Muadhamu.

Duru ya pili ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu inafanyika katika mikoa 15 nchini na kwa ajili hiyo, vimetengwa vituo 11,500 vya kupigia kura katika maeneo 22 ya uchaguzi.

Kiongozi Muadhamu akipiga kura

Katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu katika eneo la mji wa Tehran, ulifanyika mchuano kati ya wagombea 3,372, ambapo wagombea 14 kati ya hao walipata kura za kutosha kuingia bungeni, na wengine 16 watapatikana leo Ijumaa katika duru ya pili ya uchaguzi huo.

Uchaguzi wa Bunge la 12 na wa Baraza la sita la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu ulifanyika kwa wakati mmoja kote nchini Iran siku ya Ijumaa ya tarehe Mosi Machi kwa ushiriki wa wananchi wa matabaka mbalimbali.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, "Kila mtu anayetaka kuchangia ustawi wa nchi na kufikiwa malengo makubwa, lazima ashiriki katika uchaguzi."

Tags