Jun 27, 2023 13:22 UTC
  • Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu wasimama Arafa, kesho ni Mina

Mmilioni ya Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu, Al Kaaba, leo wanasimama katika uwanja wa Arafa katika kilele cha ibada tukufu ya Hijja.

Wageni hao wa Mwenyezi Mungu, al Rahman, jana jioni walialala kwenye mahema huko Mina, na leo Jumanne wameshinda kwenye Mlima Arafat wakiomba dua na kunong'ona na Mola wao Muumba.

Arafa ni jina la jangwa kubwa linalopakana na mlima Jabalur Rahma ulioko kusini mashariki mwa Makka. Tangu adhuhuri ya leo Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba, wamesimama katika uwanja wa Arafa na hadithi nyingi za Kiislamu zimetaja fadhila na utukufu mkubwa wa kisimamo hicho.

Hadithi zinasema kuwa Mwenyezi Mungu SW ameifanya ardhi ya Arafa ambayo ilikuwa medani ya matukio mengi muhimu ya kihistoria, kuwa mahali pa kuwapokea wageni wake wanaokwenda Hijja na ameweka meza na karamu yake pembeni ya Jabalur Rahma.

Magharibi ya siku hii ya leo Mahujaji wataondoka uwanja wa Arafa na kuelekea Mash'arul Haram huko Mina na kujitayarisha kwa ajili na amali nyingine za Hijja, kama kulala Muzdalifa, na kufanya amali ya Jamarat (kumpiga shetani kwa mawe saba) kesho Jumatano.

Waislamu wanaokadiriwa kuwa milioni 2.3 wamekusanyika katika mji mtakatifu wa Makka nchini Saudi Arabia kwa ajili ya Hijja ya mwaka huu, ikiashiria hatua kubwa kuelekea hali ya kawaida baada ya miaka kadhaa ya janga la corona ambapo idadi ya Mahujaji ilipunguzwa sana.

Tags