Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu uhaba wa chakula barani Afrika
Maeneo mengi ya bara la Afrika mwaka huu mpya wa 2017 yataendelea kusumbuliwa na uhaba wa chakula na hatari ya baa la njaa na ukame kwa kadiri kwamba, Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi kwamba karibu watu milioni 20 hawatakuwa na usalama wa chakula katika nchi za kaskazini na mashariki mwa Afrika.
Taasisi za misaada ya kibinadamu za Umoja wa Mataifa zimetangaza kuwa, karibu watu milioni 20 katika nchi za Afrika wanahitajia misaada ya dharura ya chakula na kwamba hakuna matarajio kuwa mahitaji hayo yatakidhiwa katika miezi kadhaa ijayo.
Ripoti iliyotolewa na Idara ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa kuhusu athari mbaya mvua kali katika maeneo ya kaskazini na mashariki mwa Afrika inasema kuwa, mavuno yasiyokuwa mazuri ya mazao ya kilimo katika miezi ya Aprili na Mei mwaka huu yataboresha kwa muda hali ya upatikanaji wa chakula katika maeneo hayo ya Afrika lakini kwa mujibu wa tathmini na makadirio ya kitaalamu, uhaba wa chakula katika nchi za Afrika katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai utashadidi tena na wakazi wa nchi hizo watakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa chakula.
Mvua kali zilizonyesha katika eneo la mashariki mwa Afrika mwishoni mwa mwezi Aprili zimesababisha mafuriko makubwa na kuathiri maisha ya zaidi ya watu nusu milioni wa eneo hilo. Ripoti ya Idara ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa, mvua hizo zimeboresha kiasi hali ya mambo kwa muda katika maeneo kama Ethiopia na Somalia ambayo yameathiriwa na ukame mkali na wa muda mrefu wa miongo kadhaa iliyopita lakini hali hiyo haitaendelea kwa kipindi kirefu na wala haitakuwa na taathira katika kuondoa athari mbaya za ukame mkubwa uliosababishwa na majanga ya kimaumbe kama yale ya El Nino.
Mabadiliko ya hali ya hewa, vita, machafuko ya ndani na kuongezeka harakati za kigaidi vimeziathiri zaidi nchi za Afrika. Kwa sasa nchi kama Ethiopia, Zimbabwe, Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini zinasumbuliwa na uhaba wa chakula. Machafuko na mivutano ya kisiasa katika baadhi ya nchi za Kiafrika na vilevile kupungua kwa pato la serikali vimezidisha umaskini na hali mbaya ya kimaisha. Haya yote yanatokea sambamba na nchi za Magharibi zinazodai kujali ubinadamu zikikataa kutimiza ahadi zao na kutoa fungu la misaada ya kifedha kwa taasisi za kimataifa za misaada ya kibinadamu ambazo sasa zinazumbuliwa na uhaba wa fedha kwa ajili ya kudhamini chakula, dawa na mahitaji mengine ya kimsingi ya wanadamu wanaosumbuliwa na matatizo ya aina mbalimbali.
Mwaka uliopita viongozi na wawakilishi wa nchi mbalimbali duniani walioshiriki katika mkutano wa Paris, Ufaransa walichukua jukumu la kupunguza athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa kupitia njia ya kufanyia mabadiliko sera na siasa zao na kutoa misaada zaidi kwa nchi zilizoathiriwa na hali hiyo. Hata hivyo kuna hatari kwamba nchi nyingi kubwa zilizoshiriki katika mkutano huo hazitatekeleza ahadi na makubaliano ya Paris. Kwa mfano tu rais mteule wa Marekani, Donald Trump ametangaza kuwa hataheshimu makubaliano ya hali ya hewa ya Paris.
Kwa msingi huo inazatamiwa kuwa, nchi nyingi za ulimwengu wa tatu hususan zile za Afrika zitakabiliwa na hali mbaya ya umaskini na njaa katika mwaka huu mpya na hata maafa makubwa ya kibinadamu iwapo jamii ya kimataifa haitachukua hatua za maana za kudhamini mahitaji ya njaa