Kuongezeka hukumu za kifo dhidi ya wapinzani nchini Saudi Arabia
Mahakama kuu ya utawala wa Aal Saud nchini Saudi Arabia imewahukumu adhabu ya kifo wanaharakati 14 kwa kushiriki katika maandamano kwenye eneo la Waislamu wa Kishia la Qatif mwaka 2011.
Ripoti zinasema kuwa, vijana hao walihukumiwa katika mahakama maalumu ya kushughulikia mafaili ya kesi za ugaidi ambapo kwa mujibu wa wanasheria ni kuwa, mahakama hiyo ni wenzo wa utawala wa Saudia wa kufikia malengo yake ya kuwakandamiza wapinzani. Yapata miaka takriban mitatu sasa, tangu utawala wa Saudia ulipopasisha sheria eti ya "Kupambana na Ugaidi" ambapo uhalifu dhidi ya binadamu katika nchi hiyo ya Kiarabu umeongezeka mno kwa kisingizio cha vita dhidi ya ugaidi. Viongozi wa Riyadh wakitumia kisingizio hicho wamekuwa wakihalalisha ukandamizaji wao dhidi ya wananchi wa nchi hiyo.
Ukweli wa mambo ni kuwa, watawala wa Saudi Arabia daima wakiwa na lengo la kukandamiza uhuru wa kujieleza au uhuru wa kutoa maoni wamekuwa wakitumia suala la kupambana na ugaidi na hivyo kutoa adhabu kali kwa raia. Maeneo mbalimbali ya Saudi Arabia hususan yale ya mashariki mwa nchi hiyo likiwemo eneo la Qatif kuanzia mwaka 2011 hadi sasa yamekuwa yakishuhudia malalamiko ya kupinga dhulma na kutaka kuweko ugawaji wa kiadilifu wa utajiri wa nchi hiyo. Vikosi vya usalama vya Saudi Arabia vimekuwa vikivamia mara kwa mara maeneo tofauti ya mkoa wa Sharqiyyah mashariki mwa nchi hiyo ambapo sambamba na kushambulia nyumba za raia vimekuwa vikimwaga damu za raia hao na kuwatia mbaroni wanaharakati wa kisiasa.
Hii ni katika hali ambayo, siasa za kuzusha mifarakano na uporaji zimeyafanya maisha ya wananchi hao kuwa magumu hususan katika mkoa wa Sharqiyyah ambao wakazi wake ni Waislamu wa madhehebu ya Ahlu-Baiti. Utawala wa Saudi Arabia umejidhihirisha wazi kwamba dhati yake ni kuwafarakanisha Waislamu. Hii ni kutokana na kuwa, utawala wa Aal Saud umejengeka juu ya fikra potofu za Kiwahabi, fikra ambazo zimeleta madhara makubwa kwa Waislamu.
Uwahabi una fikra mgando na hii ni sifa mbaya ambayo imo katika muundo wa utawala wa Aal Saud nchini Saudia. Katika kalibu hii, Waislamu wa Kishia nchini Saudi Arabia ambao ni kundi la wachache lakini walioenea kwenye maeneo yenye utajiri mkubwa wa mafuta ya nchi hiyo, kwa mujibu wa mtazamo wa utawala wa Riyadh, raia hao hawastahiki kupewa haki sawa na raia walio wengi ambao ni wafuasi wa madhehebu nyingine. Ni kwa muktadha huo, ndio maana Mashia nchini Saudia wamekuwa wakihesabiwa kuwa ni raia wa daraja la pili. Ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya kundi hili la raia wa Saudia unaofanywa na utawala wa kifamilia wa Aal Saud ni mkubwa kiasi kwamba, hata baadhi ya wachambuzi wa mambo na wananadharia wamewapa jina la kupanga raia hao kwa kuwaita ni "Waislamu Waliosahaulika".
Hii ni katika hali ambayo, Waislamu wa Kishia nchini Saudia wanasisitiza kuheshimiwa utambulisho wao wa kitaifa na mara chungu nzima wamekuwa wakiandamana wakitaka kupatiwa haki sawa na raia wengine wa nchi hiyo. Watawala wa Aal Saud kama walivyo akthari ya watawala wa Ghuba ya Uajemi, daghadagha yao kuu ni kulinda utawala wao. Wasiwasi huo huo umeshtadi hasa baada ya kuongezeka malalamiko ya wananchi dhidi yao, hivyo wameamua kuwasukumia tuhuma mbalimbali raia hao kama vile kuunga mkono ugaidi au kupata miongozo kutoka nje.
Kwa mintarafu hiyo, idadi kubwa ya wapinzani wametiwa mbaroni na kushikiliwa kwa miezi mingi au hata miaka pasina ya kuhukumiwa. Baadhi yao wamepandishwa kizimbani na kukatiwa vifungo vizito au hata adhabu ya kifo. Wachambuzi wa mambo wanaashiria dhulma, ukandamizaji na ukosefu wa uadilifu katika utoaji hukumu nchini Saudia na kusisitiza kwamba, nchi hiyo inaendeshwa kwa misingi ya itikadi za utumiaji mabavu za Kiwahabi.