Mwito wa Libya wa kuondolewa vikwazo vya silaha
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i37053-mwito_wa_libya_wa_kuondolewa_vikwazo_vya_silaha
Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya ametaka nchi yake iondolewe vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2011.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 02, 2017 00:42 UTC
  • Mwito wa Libya wa kuondolewa vikwazo vya silaha

Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya ametaka nchi yake iondolewe vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2011.

Fayez Sarraj ametoa mwito huo mjini Washington wakati alipoonana na James Mattis, waziri wa ulinzi wa Marekani. Amesema Libya imekumbwa na changamoto mpya zinazosababishwa na misimamo mikali na ugaidi na kuelezea matumaini yake kwamba vikwazo vya silaha dhidi yanchi yake vitaanza kuondolewa pole pole kwa baadhi ya makundi ya ulinzi ya nchi hiyo kama vile gadi ya ulinzi wa rais na gadi ya ulinzi wa fukweni.

Mapigano baina ya makundi hasimu ni jambo la kawaida nchini Libya

 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliiwekea vikwazo vya silaha Libya baada ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kukumbwa na machafuko ya kisiasa mwaka 2011. Mwaka huo Baraza la Usalama lilipasisha azimio nambari 1970 ambalo lilizipiga marufuku nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuiuzia silaha Libya.

Hivi sasa waziri mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya yuko mjini Washington katika hali ambayo mgogoro ulioikumba nchi yake umechochewa na siasa za Marekani na waitifaki wake walioivamia kijeshi Libya na baadaye kuitelekeza huku silaha zikiwa zimetapakaa mikononi mwa watu na makundi hasimu. 

Ni hivi majuzi tu ambapo Mohammad al Hanqari, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Libya alifichua mpango wa siri wa Marekani wa kuidhibiti nchi hiyo. Alisema: "Marekani kwa kushirikiana na baadhi ya nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inafanya njama za kuhodhi uendeshaji wa Libya mikononi mwa umoja huo katika kipindi hiki cha mpito."

Viongozi wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya wanaamini kuwa, vikwazo vya silaha ilivyowekewa nchi hiyo vimevidhoofisha sana vikosi vyake vya ulinzi na kutoa mwanya wa kupata nguvu magenge ya wanamgambo. Viongozi hao wanasema kuwa, serikali ya Libya haiwezi kupambana na magenge ya kigaidi hadi pale itakapokuwa na silaha za kutosha. Wanasema silaha zilizopo hivi sasa hazitoshi, bali sehemu kubwa ya silaha hizo ziko mikononi mwa makundi tofauti ya wanamgambo.

Marufuku ya silaha haiyazuii magenge ya kigaidi kumiliki silaha za kila namna nchini Libya

 

Hivi karibuni, Mahdi Saleh Al-Mijribi, mwakilishi wa kudumu wa Libya katika Umoja wa Mataifa alisema kuwa: "Tunaiomba jamii ya kimataifa iondoe marufuku ya kutumwa silaha nchini Libya na iruhusu vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo kutumiwa zana za dharura za kijeshi ambazo zitasaidia sana katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi."

Hata hivyo, nchi zinazotekeleza vikwazo vya silaha dhidi ya Libya zinadai kuwa kama nchi hiyo itaruhusiwa kununua silaha, basi makundi ya wanamgambo yatapata nguvu nchini humo hivyo hadi hivi sasa zimekuwa zikikwepa kuiuzia silaha Libya. Jambo hilo linafanyika katika hali ambayo hivi sasa Libya iko katika moja ya njia kuu za usafirishaji kimagendo wa silaha kuelekea nchi mbalimbali na sasa hivi imegeuka kuwa soko kuu la kuuzia silaha hizo. Magaidi na makundi ya wanamgambo wenye misimamo mikali yanamiliki silaha nchini Libya hivi sasa na yanapata silaha hizo kwa njia za magendo.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kitendo cha kuwekewa vikwazo vya silaha Libya kwa upande mmoja ni hatua ya kukukuza na kuchochea mgogoro nchini humo, kwani udhaifu wa serikali ndio unaifanya ishindwe kuyadhibiti magenge yenye silaha; na  kwa upande wa pili, mambo hayo yaliviandalia fursa nzuri viwanda vya silaha hasa vya Magharibi kuuza silaha kwa bei za juu katika kona mbalimbali za dunia kwa kutumia ukosefu wa utulivu nchini Libya. Wachambuzi hao wanasema, mambo kama hayo ndiyo yanayokwamisha juhudi za kuutafutia utatuzi wa kisiasa mgogoro wa Libya na kupelekea kuwa vigumu sana kufanikiwa.