Maktaba ya Imam Khomeini (MA) na sauti-1
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya kwanza ya kipindi hiki kipya cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Kipindi hiki ni miongoni mwa vipindi 32 ambavyo vitajikita katika kuarifisha shakhsia na sira ya Imam Khomein (MA), Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Aidha katika kipindi hiki tutabainisha msingi wa mapambano dhidi ya ubeberu katika usia wa Mapinduzi ya Kiislamu hivyo tunakukaribisheni kusikiliza mfululizo wa vipindi hivi hadi mwisho wake, karibuni.
Ndugu wasikilizaji, hatua ya Imamu Khomeini (MA) ya kufuata mafundisho asili ya Kiislamu, sira ya kivitendo ya Mtume Muhammad (saw), Imam Ali (as) na kwa uungaji mkono wa wananchi ilimuwezesha kung'oa mfumo wa kidikteta uliokuwa umekita mizizi katika jamii ya Iran. Ni kupitia Mapinduzi ya Kiislamu, ambapo hii leo na tukiwa tunaadhimisha miaka 40 ya mapinduzi hayo, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unaonekana kuwa na thamani ya kipekee kwa Wairani. Mambo hayo ndiyo yamepelekea kuandaliwa kipindi hiki ili nanyi muweze kunufaika na yale ambayo mlikuwa hamyafahamu katika maktaba hii. wapenzi wasikilizaji katika sehemu ya kwanza ya kipindi hiki a kama tulivyotangulia kusema, tutazungumzia mapambano ya Imam Khomeini (MA) dhidi ya ubeberu.
Mtafahamu kwamba akthari ya wanafikra na weledi wa masuala ya kisiasa, wameyatofautisha Mapinduzi ya Kiislamu na mapinduzi mengine duniani. Wakizungumzia uhalisia wa Mapinduzi ya Kiislamu weledi hao wameashiria nukta ambazo hazipatikani katika mapinduzi mengine ya duniani. Kwa mfano tu baadhi ya wanafikra hao wameitaja nukta ya dini kuwa moja ya mambo yaliyoyatofautisha Mapinduzi ya Kiislamu nchini hapa na mapinduzi mengine huku wakiashiria kwamba, Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yalifikia kilele katika kipindi ambacho katika maeneo mengi ya dunia, dini ya Kiislamu ilikuwa imeondolewa katika ulingo wa kisiasa. Katika uwanja huo, viongozi wa kiroho na asasi za kidini hawakutakiwa kujihusisha na masuala ya kisiasa. Mbali na hayo ni kwamba baadhi ya mirengo ya kifikra na kifalsafa kama vile nadharia ya Umaksi ziliitaja dini kuwa ni afyuni ya umati wa watu, kwa kuwa kwa mujibu wa fikra hizo, dini ilikuwa ndiyo iliyowaunganisha wananchi katika kukibiliana na dhulma ya kimatabaka iliyotawala. Hata hivyo Mapinduzi ya Kiislamu na kwa mtazamo wa mafundisho ya dini ya Uislamu na madhehebu ya Shia, yalifanikiwa kuwaunganisha Wairan dhidi ya dhulma ya kimatabaka iliyokuwa ikitawala na hivyo kuunda mfumo mpya ambao ulilingania uadilifu wa kijamii pamoja na uhuru. Kupambana na ubeberu pia ni moja ya sura nyingine zilizoyatofautisha Mapindizi ya Kiislamu na mapinduzi mengine duniani. Hii ni kwa kuwa mapambano hayo dhidi ya ubeberu yalitokana na mafundisho yale yale ya dini ambayo pia ndio msingi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
**********
Ili kufahamu vyema madhumuni ya mapambano dhidi ya ubeberu yaliyosisitizwa na Mapinduzi ya Kiislamu, ni lazima kwanza tutazame kipindi ambacho mapinduzi hayo yalifikia kilele. Wapenzi wasikilizaji Mapinduzi ya Kiislamu yalifikia kilele wakati ambao ulimwengu ulikuwa unaongozwa na kambi mbili kuu, huku nchi nyingi zikiungana na moja ya kambi hizo. Katika kipindi cha vita baridi au wakati wa msuguano wa kambi hizo mbili, kama ilivyo leo, Marekani ilikuwa ikiongoza kambi ya Magharibi au mfumo wa kibepari, huku kwa upande mwingine Urusi ya zamani ikiongoza kambi ya Mashariki na mielekeo yote ya Ukomonisti. Katika anga hiyo kulikuwa na ushindani mkubwa na mkali sana ambapo hata wakati mwingine uliibua uwezekano wa kuzuka mapigano ya nyuklia. Aidha nchi zote za ulimwengu wa tatu zilikuwa zikifanya uhusiano wao na kambi hizo mbili ambapo mabadiliko yaliyokuwa yakitokea ndani ya nchi hizo, yalikuwa yana uhusiano wa moja kwa moja na irada ya viongozi wa kambi hizo kuu mbili. Katika kipindi hicho, mapinduzi mengi yaliyotokea, yalifungamana na fikra za mrengo wa kushoto, kwa kuwa kambi ya Ukomonisti iliandaa zaidi fursa za kufanyika mapinduzi. Ni katika mazingira hayo ndipo, Mapinduzi ya Kiislamu yalifikia ushindi nchini Iran chini ya kaulimbiu ya ‘Si Mashariki, wala Magharibi’ sambamba na kusisitiza juu ya malengo matukufu ya ‘kujitawala’ na hivyo mapinduzi haya yakawa yamepinga kwa wakati mmoja, ubeberu wa madola mawili yenye nguvu wakati huo yaani Marekani na Urusi ya zamani.
*************
Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni Maktaba ya Imamu Khomein hii ikiwa ni sehemu ya kwanza ya mfululizo huu.
Kupambana na ubeberu ni moja ya mihimili ya malengo ya Maktaba ya Imam Khomeini (MA) na pia kaulimbiu ya Mapinduzi ya Kiislamu. Suala hilo linatokana na mtazamo wa chimbuko la dini ya Imam Khmeini. Hii ni kusema kuwa, katika dini ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu ya Imam Khomeini, mfumo wa uumbaji ni wa ‘msingi mmoja’ na Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye msimamizi wake. Katika uwanja huo viumbe wote wanapatikana chini ya irada ya Mwenyezi Mungu kama ambavyo pia dunia umeumbwa kwa uwezo wake yeye Allah. Kwa mujibu wa fikra hiyo, viumbe wote duniani ni dhaifu mbele ya Mwenyezi Mungu na wote wanatakiwa kufuata amri yake Yeye. Kwa msingi huo, iwapo kiumbe yeyote na kwa jeuri yake atatoka kwenye mstari wa kumtii Mwenyezi Mungu na wakati huo huo akajiona kuwa mwenye kujitosheleza na kujitoa katika fremu ya kiumbe wa Mungu, basi atatambulika kuwa aliyeasi na mwenye kiburi (beberu). Kwa mtazamo huo, shetani ndiye kiumbe wa kwanza mwenye kibri katika historia ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu kwa kuwa aliasi na kukengeuka amri za Mwenyezi Mungu. Kadhalika, hata baada ya Nabii Adam (as) kuterenshwa duniani na kuanza maisha ya kibinaadamu kwenye uso wa dunia hii, pia kumekuwepo na kundi la watu ambao mara zote wamekuwa wakimfuata shetani katika kufanya kibri sambamba na kuwakandamiza mawalii wa Mwenyezi Mungu na watu wa kawaida. Kwa mujibu wa Imam Khomeini, katika jamii zote na katika mifumo yote ya dunia, kuna matabaka mawili ya watu mabeberu (watu wenye jeuri) na watu dhaifu, hivyo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu yamesimama kwenye msingi wa kupambana na mabeberu na kuwasaidia watu dhaifu.
*********
Ni kwa kutegemea mafundisho hayo sambamba na ukandamizaji wa ndani na dhulma iliyokuwa ikitawala, ndipo Imam Khomeini akasimama na kuongoza jihadi (mapambano) dhidi ya mfumo wa kibeberu uliokuwa unatawala dunia, yaani kambi mbili za Marekani na Urusi ya zamani ambapo kufuatia kuushindwa mfumo wa ukandamizaji uliokuwa unatawala nchini Iran, akawa pia amepeperusha bendera ya mwamko wa kukabiliana na ubeberu wa dunia kote ulimwenguni. Katika uwanja huo, Imam Khomeini hakuchukulia kuwa mapambano dhidi ya ubeberu yaliishia katika mipaka ya kijografia ya Iran bali msaada wake wa kuwatetea watu dhaifu, uliwahusu watu wote wa dunia. Kuhusiana na suala hilo aliamini kwamba, katika daraja la kwanza ndani ya mamlaka ya Kiislamu, watu wote wanaodhulumiwa wanatakiwa kuungana kwa pamoja sambamba na kusimama kwa ajili ya kuendesha mapambano dhidi ya mabeberu. Imamu Khomeina (MA) anasema: “Tunataka nchi zote za Kiislamu ziwe na sifa hiyo, na hii ina maana kwamba, kwa kuwa imethibiti nchini Iran hivyo inatakiwa pia ithibiti katika nchi zote za Kiislamu sambamba na wanyonge wote duniani kusimama kwa ajili ya kupambana na mabeberu, kutatua matatizo yao na hatimaye kurejesha haki yao. Ni lazima wafahamu kwamba ili kupata haki yao ni lazima waipiganie na huwawezi kuipata haki hiyo kwa urahisi.” Mwisho wa kunukuu.
Wapenzi wasikilizaji sehemu ya kwanza ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.