Sheikh Naim Qassim: Kamwe muqawama hautasalimisha silaha zake
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129570
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa , kamwe Kamwe muqawama hautasalimisha silaha zake. 
(last modified 2025-08-15T11:17:09+00:00 )
Aug 15, 2025 11:17 UTC
  • Sheikh Naim Qassim: Kamwe muqawama hautasalimisha silaha zake

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa , kamwe Kamwe muqawama hautasalimisha silaha zake. 

Sheikh Naim Qassim ameeleza kuwa, Palestina itasalia kuwa mwelekeo wa dira na kwamba mauaji ya halaiki hayatawazuia wananchi wa Palestina kuendelea na muqawama wao.

Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema hayo katika hotuba yake katika kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein (AS) huko Baalbek, Lebanon na kubainisha kwamba, leo tunaweka maisha yetu, mustakabali na vizazi vyetu katika msingi wa kwamba kila ardhi na wakati ni kwa ajili ya ushindi, kujitolea kufa shahidi na kufikia malengo makubwa.

Alifafanua kwamba tunasimama pamoja na kuunga mkono muqawama na Palestina na dhidi ya Yazid wa zama, ambao ni Marekani na Israel. Daima tutasimama kwenye ukweli na haki.

Silaha za Harakati ya Mapambano ya Hizbullah ya Lebanon zimekuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na uvamizi wa Israel dhidi ya ardhi ya Lebanon

 

Katibu Mkuu wa Hizbullah aliendelea kwa kusema kwamba, muqawama ni matokeo na zao la shule ya Karbala na maisha ya taifa la Kiislamu.

Kiongozi huyo wa Hizbullah ya Lebanon amesifu uungaji mkono usioyumba wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na misimamo yake ya kijasiri kwa muqawama.

Suala la kupokonywa silaha harakati ya Hizbullah nchini Lebanon ni mpango wa Marekani uliotwishwa kwa serikali ya Beirut. Mpango huo uliwasilishwa na Tom Barak, mjumbe wa kikanda wa Rais wa Marekani, Donald Trump. Kwa mujibu wa mpango huo wa hatua nne, Hizbullah inapaswa kupokonywa silaha ifikapo mwisho wa 2025.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, uamuzi wa serikali ya Lebanon wa kutaka kuipokonya silaha Hizbullah unaweza kuzidisha migawanyiko ya kisiasa nchini humo na hata kuibia tena mapigano ya umwagaji damu ya mwaka 2008.