Kuendelea mashambulio ya kijeshi ya Uturuki dhidi ya Syria na Iraq
(last modified Fri, 04 Aug 2023 02:32:07 GMT )
Aug 04, 2023 02:32 UTC
  • Kuendelea mashambulio ya kijeshi ya Uturuki dhidi ya Syria na Iraq

Licha ya kufanyika mazungumzo ya amani kati ya Ankara na Damascus, mashambulizi ya kijeshi ya Uturuki dhidi ya Syria na Iraq yangali ni ajenda inayofanyiwa kazi na serikali ya Ankara.

Kuhusiana na suala hilo, Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imetangaza katika taarifa kuwa, wanajeshi wa Uturuki wamewaua wanachama 12 wa kundi la YPG katika eneo la operesheni la jeshi la nchi hiyo kaskazini mwa Syria, linalojulikana kama eneo la operesheni la Ngao ya Furat (Euphrates Shield). Huku hayo yakijiri, kwa mara nyingine tena ndege za kivita za Uturuki zimeshambulia maeneo kadhaa ya mji wa Dohuk kaskazini mwa Iraq na kusababisha hasara kubwa kwa ardhi za kilimo za mji huo. Hakukuwa na ripoti zilizotolewa kuhusu idadi ya watu ambao huenda waliuawa katika shambulio hilo la anga.

Wakati huo huo vyombo vya habari vya Uturuki vimetangaza kuwa wanachama wanne wa Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan cha Uturuki (PKK) wameuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za jeshi la nchi hiyo katika eneo la Kurdistan ya Iraq.

Kwa kawaida, mashambulizi ya jeshi la Uturuki ndani ya ardhi za Syria na Iraq huwa yanaambatana na maafa ya roho za watu, wakiwemo wanaume raia kawaida, wanawake na watoto wadogo sambamba na kusababisha pia hasara nyingi za kiuchumi. Pamoja na hayo, taarifa zinazotolewa na jeshi la Uturuki kila mara huwa zinasisitiza kuwa wanajeshi wake wameweza kufikia malengo waliyokusudia katika ardhi za Syria na Iraq.

Jeshi la Uturuki

 

Katika miaka michache iliyopita, wanajeshi wa Uturuki wamekuwa kila mara wakitoa ripoti kama hizo. Lakini licha ya hayo, ukweli unaonyesha kuwa jeshi la Uturuki lingali lipo palepale lilipokuwa. Sambamba na kutekeleza kile kinachoitwa operesheni ya Ngao ya Furati nchini Syria, jeshi la Uturuki ilianzisha pia operesheni inayoitwa Kufuli la Kucha (Claw Lock) nchini Iraq. Mnamo Aprili 18, 2022, ndipo Uturuki ilipoanza kutekeleza operesheni hiyo ya Kufuli la Kucha kaskazini mwa Iraq.

Wataalamu wa masuala ya eneo wanaamini kuwa mashambulizi ya Waturuki katika ardhi za Syria na Iraq yanatokana na sera za tamaa na kupenda kujitanua za viongozi wa serikali ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, kuhusiana na nchi hizo. Hii ni pamoja na kwamba, maafisa wa serikali ya Ankara wameshatoa mara kadhaa kauli za kutafakarisha juu ya suala hilo. Kwa mfano rais Erdogan mwenyewe amekuwa akidai kila mara kwamba nchi yake haizimezei mate wala kuziangalia kwa jicho la tamaa ardhi za Syria na Iraq. Lakini hilo ndilo linaloshuhudiwa kivitendo katika hatua zinazochukuliwa na viongozi wa serikali ya Ankara kuhusiana na ardhi za nchi hizo mbili jirani.

Kwa namna ya kutafakarisha, viongozi wa serikali ya Ankara hivi karibuni wamebadilisha misimamo yao kuhusiana na suala la kuanzisha uhusiano na Syria wakati wakiwa wako katika mazungumzo na Damascus. Kwa mfano, rais Erdogan wa nchi hiyo hivi karibuni alisema: "kuna kila uwezekano, ikiwa ni pamoja na kukutana na yeye Rais wa Syria Bashar Assad. Rais wa Syria anatutaka tuondoke katika ardhi ya kaskazini mwa nchi hiyo. Lakini Uturuki haiwezi kutimiza sharti kama hilo, kwa sababu iko kwenye vita vya kupambana na ugaidi na inakabiliwa na kitisho kutokea eneo hilo." Kwa hakika, kauli anazotoa Rais wa Uturuki zinaonyesha mgongano mkubwa katika sera za nchi hiyo kwenye uga wa uhusiano wake na nchi jirani, hususan Syria.

Wapiganaji wa Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan cha Uturuki (PKK)

 

Alexander McKeever, mtaalamu na mchunguzi wa masuala ya Syria amesema yafuatayo katika kueleza sababu inayolifanya suala la kurejeshwa uhusiano kati ya Ankara na Damascus lisitekelezeke: "Bashar Assad ameiomba Uturuki iondoe majeshi yake katika ardhi ya Syria, lakini Uturuki imekataa kutekeleza takwa hilo; kwa sababu inaitakidi kwamba ikiwa itaondoka katika ardhi za kaskazini mwa Syria, mamilioni ya wakazi wa maeneo hayo yanayokaliwa na Uturuki watakimbilia kwenye mipaka ya Uturuki na kumiminika ndani ya ardhi ya nchi hiyo”.

Ukweli ni kwamba, katika kipindi cha miaka michache iliyopita, maafisa wa serikali ya Erdogan wamejaribu kuvizatiti vikosi vya wapiganaji wanaoipinga serikali ya Bashar al-Assad vilivyoko ndani ya ardhi ya Syria ili kuwatumia kwa manufaa ya Uturuki. Ifahamike pia kwamba maafisa wa serikali ya Erdogan wameyajumuisha makundi ya Wakurdi, kikiwemo Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan wa Uturuki (PKK) na Jeshi la Ulinzi la Watu wa Syria (YPG) kwenye orodha yake ya makundi ya kigaidi.

Lakini mbali na hatua za kijeshi inazochukua ndani ya Uturuki yenyewe, Ankara inayashambulia kinyume cha sheria maeneo ya kaskazini mwa Iraq na Syria pia kwa kisingizio cha kupambana na makundi hayo, suala ambalo limekuwa likilaaniwa na kupingwa vikali kila mara na wananchi na serikali za nchi hizo mbili, na kutoa wito wa kukomeshwa hujuma hizo za kivamizi. Licha ya malalamiko yote hayo, jeshi la Uturuki lingali linazikalia kwa mabavu na kinyume cha sheria ardhi za Syria na Iraq. Pamoja na kauli mbiu zinazoonekana kuwa za kupenda suluhu na amani zinazotolewa na viongozi wa Ankara, ni baidi kwamba matatizo ya Uturuki na majirani zake hao wawili yatamalizika katika muda mfupi ujao…/