Hamas: Kadhia ya Palestina inakabiliwa na changamoto ya aina yake
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imeeleza kuwa suala la Palestina linakabiliwa na changamoto ambayo haijawahi kushuhudiwa.
Usama Hamdan mjumbe wa ngazi ya juu wa Hamas amesema kuwa: Katika kikao cha Cairo imebainika kuwa kadhia ya Palestina inakabiliwa na changamoto ya aina yake, na chini ya kivuli cha serikali ya kifashisti inayoongozwa na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuna ulazima wa kuwepo maamuzi ya pamoja baina ya Wapalestina.
Katika mashauriano aliyofanya na makatibu wakuu wa makundi na harakati za kupigania uhuru wa Palestina huko Cairo nchini Misri, Usama Hamdan amesema: Hamas inazingatia aina zote za mapambano na kwamba haikubaliki kwa mtu mmoja kuzuia aina yoyote ya muqawama. Amesisitiza kuwa, harakati hiyo inajivunia mapambano yanayoendelea katika eneo la Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan.
Mjumbe huyo wa ngazi ya juu wa Hamas ameongeza kuwa, wajibu wao wa kitaifa ni kuimarisha mambo yote yanayopanua zaidi mapambano ya ukombozi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi, na kwamba yeyote anayezuia silaha kuwafikia wanamapambano huko katika Ukingo wa Magharibi ni mtenda jinai.
Kuhusiana na hilo, awali makundi manane ya Wapalestina katika taarifa yao ya pamoja yaliitaka Mamlaka ya Ndani ya Palestina kusitisha kuwatia mbaroni kisiasa Wapalestina huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Mamlaka ya Ndani ya Palestina haya hivyo inaendelea kuwatia nguvuni viongozi na wanachama wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina huko Ukingo wa Magharibi.
Baadhi ya wawanamapambano wa Kipalestina, kama Murad Walid Malashieh na Mohammad Walid Barahimah kutoka katika mji wa Jenin, bado wako gerezani licha ya mahakama kutoa uamuzi kwamba wanapaswa kuachiliwa huru mara moja.