Israel yateketeza mahema kwenye Hospitali ya Ghaza na kuwachoma moto Wapalestina wakiwa hai
(last modified 2024-10-14T06:12:02+00:00 )
Oct 14, 2024 06:12 UTC
  • Israel yateketeza mahema kwenye Hospitali ya Ghaza na kuwachoma moto Wapalestina wakiwa hai

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limeishambulia kwa mabomu kambi ya wakimbizi katika eneo la kati la Ukanda wa Ghaza na kusababisha moto mkubwa uliopelekea kuuawa shahidi Wapalestina waliokuwa wametafuta hifadhi kwenye eneo hilo kutokana na hilaki ya vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na utawala huo ghasibu.

Mashambulizi hayo yaliyofanywa mapema leo, yamelenga kambi iliyowahifadhi Wapalestina waliolazimika kuyahama makazi yao na kukimbilia kwenye uwanja wa Hospitali ya Mashahidi wa al-Aqsa katika mji wa Deir al-Balah, na kuua watu wasiopungua wanne na kujeruhi wengine wapatao 70.
 
Wizara ya Afya ya Ghaza imesema idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka huku kukiwa na hofu kuwa makumi ya Wapalestina waliolazimika kuyahama makazi yao watakuwa wameuawa shahidi katika hujuma hiyo.
 
Picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha watu wakijaribu kuzima moto huo kwa kutumia chochote walichokuwa nacho, ikiwa ni pamoja na mablanketi na ndoo za maji.

Vyombo vya habari vya lugha ya Kiarabu vimeonyesha picha na taswira za kutisha za maafa ya mashambulizi yaliyoilenga kambi hiyo, wakati wakazi wake wengi wakiwemo watoto wakiwa wamelala.

Jeshi la utawala wa Kizayuni limedai kuwa lilifanya mashambulizi hayo yalilenga 'kamandi ya kijeshi' inayotumiwa na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina, Hamas.

Hata hivyo Hamas imekanusha vikali madai hayo ambayo hutumiwa mara kwa mara na utawala wa Kizayuni ili kujaribu kuhalalisha vitendo vyake vya kinyama dhidi ya raia wa Palestina.

Mashambulizi hayo ya leo yanafuatia mauaji mengine yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni, ambapo Wapalestina wapatao 20 wakiwemo watoto, wameuliwa shahidi ndani ya kambi ya wakimbizi ya Nuseirat, katikati ya Ghaza.../

Tags