Mamia ya wafungwa Bahrain wagoma kula wakilalamikia hali mbaya ya magereza
Duru za Bahrain zimetangaza kuwa, mamia ya wafungwa wa utawala wa Al-Khalifa wamegoma kula wakilalamikia hali mbaya ya jela.
Jumuiya ya al-Wefaq ya Bahrain imetangaza leo Ijumaa kwamba mamia ya wafungwa wa Bahrain wamegoma kula wakilamikia hali ngumu ya magereza ikiwa ni pamoja na kuwekwa ndani ya seli kwa muda wa saa 23 kwa siku na kuzuiwa kufanya shughuli za kidini.
Mwanaharakati wa masua la sheria wa Bahrain, Ebtisam Al-Sayegh ametangaza kwamba idadi ya wafungwa wa kisiasa nchini Bahrain hivi sasa inazidi watu elfu mbili ambao wanaishi katika mazingira magumu sana.
Al-Sayegh amesema, inasikitisha kwamba, hali za wafungwa pia ni mbaya na zinazoandamana na ukatili. Amesema wafungwa hao wananyimwa haki za msingi kabisa, utu wao unadhalilishwa, wanaishi katika mateso ya kiakili na kimwili, na baadhi yao wanakufa taratibu kutokana na maradhi na kukosa huduma ya matibabu.
Ahmed Al-Wadaei, mkuu wa Taasisi ya Sheria na Demokrasia ya Bahrain, amesema kuwa wafungwa hao wananyimwa haki zao za kufanya shughuli za kidini kwa miaka mingi na hawana haki ya kuondoka katika seli zao kwa muda mrefu.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakiilaani serikali ya Bahrain kwa kuwakandamiza wapinzani na yametoa wito wa kufanyika marekebisho katika mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo.